Hiyo ndiyo kweli isiyo na shaka yoyote. Kwani hapanapo mungu ila Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu, na Yeye ni pekee katika utukufu wa Ufalme wake na hikima katika uumbaji wake.
Sema, ewe Nabii! Enyi Watu wa Kitabu! (Biblia, yaani Mayahudi na Wakristo) njooni kwenye neno moja la uadilifu lenye kutukusanya sote na tunalo litaja, nalo ni kuwa hatumuabudu ila Mwenyezi Mungu tu, wala tusimwekee washirika katika ibada. Na wala tusiwe tunawat'ii baadhi yetu tukiwafuata katika kuhalalisha na kuharimisha, tukaachilia mbali hukumu ya Mwenyezi Mungu katika mambo ya halali na haramu. Wakiukataa wito huu wa haki waambie: Shuhudieni kuwa sisi ni Waislamu, yaani tunafuata hukumu za Mwenyezi Mungu, na Yeye tu tumemsafia Dini, wala hatumwombi mwengineyo. (Taurati:Kutoka 20.3:Usiwe na miungu mingine ila Mimi. Injili ya Marko 12.29 : Yesu akamjibu, [amri] Ya kwanza ndiyo hii, Sikia Israel, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja.)
Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnazozana na kujadiliana kwa mambo ya Ibrahim, kila mmoja wenu akidai kuwa yeye ndiye anaishika dini yake, na ilhali Ibrahim alikuwako kabla ya Taurati na Injili akifuata sharia mbali. Hizo Taurati na Injili hazikuja ila baadae. Basi atakuwaje yeye afuate sharia za vitabu hivyo? Hamna akili ya kutambua jambo hili lilio wazi?
Watu nyinyi mlikuwa mkijadili mambo yalio wakhusu Musa na Isa mnayo yajua kama mnavyo dai wenyewe. Imekuwaje basi hivi sasa kudai kuwa Ibrahim alikuwa Yahudi au Mkristo - jambo ambalo nyinyi hamlijui! Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua hakika ya hayo mnayo gombania, na nyinyi hamjui kitu.
Hakika Ibrahim a.s. hakufuata dini ya Kiyahudi wala dini ya Kikristo, lakini ameachana na dini zote za upotovu na akashika Dini ya Haki, ya Uislamu, yaani kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kumtakasia Yeye kwa ut'iifu, na wala hakuwa miongoni wa hao wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu katika kuabudu.
Hakika wenye haki kabisa kunasibiana na Ibrahim na Dini yake ni wale walio mwitikia wito wake na wakaongoka kufuata uwongofu wake katika zama zake, na vile vile Muhammad s.a.w. na walioamini pamoja naye. Kwani hao ni watu wa Tawhidi safi ya kweli, kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja bila ya walakini. Hiyo ndiyo Dini ya Ibrahim. Mwenyezi Mungu anawapenda Waumini, na Yeye atawanusuru, kwani wao ni vipenzi vyake, na atawalipa kwa mema na ziada.
Kipo kikundi katika Watu wa Kitabu wanao tamani kuwapotoa Waumini na kuwafitini waache Dini yao, kwa kuwatilia mikorogo ya kudhoofisha itikadi. Lakini katika kazi yao hii hawatampotoa mtu ila nafsi zao wenyewe kwa kuendelea katika upotovu, ambao utakuja kuwagubika wao wenyewe tu, na wala hawajui kuwa matokeo ya juhudi yao ovu yatawapata wenyewe, wala hayatawadhuru Waumini.
Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha Aya na Ishara za Mwenyezi Mungu zilizo teremka kuthibitisha Unabii wa Muhammad, s.a.w. na hali nyinyi mnaijua haki?