Enyi Waumini! Yaliyo kusibuni lilipo pambana jeshi lenu na jeshi la Washirikina katika Uhud yametokana kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu, na ili awadhihirishie watu Imani ya Waumini ya kweli aliyo ifunza.
Na hayo ili pia udhihiri unaafiki wa wanaafiki. Nao hawa ni wale walipo kuwa wanaondoka wanaacha vita wakaambiwa: Njooni mpigane kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu, au kwa ajili ya kujilinda nafsi zenu. Wakasema: Lau kuwa tunajua kuwa mtakutana na vita, tungeli kwenda nanyi. Na wao walipo sema kauli hiyo walikuwa karibu zaidi na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao: Huko hakuna vita. Na hali wanaitakidi ndani ya nyoyo zao kuwa vita kweli vitakuwepo. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema unaafiki wanao uficha, kwani Yeye anajua matokeo ya siri zao.
Na hao ndio walio baki nyuma wesende vitani wakakwepa, na wakasema kwa mintarafu ya ndugu zao walio toka wakauliwa: Lau wangeli tufuata sisi wakakaa nyuma kama tulivyo kaa sisi wangeli okoka kama tulivyo okoka. Waambie: Zizuieni nafsi zenu basi zisife, kama mnasema kweli kuwa hadhari inazuia kadari.
Wala usidhani kabisa kuwa walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti, bali hao wahai kwa uhai anao ujua Mwenyewe Mwenyezi Mungu, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi, riziki njema anayo ijua Yeye.
Nyuso zao zinameremeta kwa furaha na bishara kwa fadhila ya pekee aliyo wapa Mwenyezi Mungu, na wanawafurahia ndugu zao ambao walio waacha duniani wangali wahai, wanashika mwendo wa Imani na Jihadi, na ya kwamba hapana khofu juu yao kupata lolote la karaha wala si wenye kuhuzunika kwa kumkosa mpendwa.
Nyuso za Mashahidi zinameremeta kwa neema ya kufa shahidi na neema ya Pepo, na ubora wa karama, na ya kwamba haupotei ujira wa Waumini.
Waumini hao ni wale ambao wameitikia wito wa Mtume wa kuanza upya Jihadi baada ya pigo kubwa walilo lipata katika vita vya Uhud. Kwa hivyo basi wakawa ni wenye kutenda wema, na wakajilinda na kuasi amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakastahiki ujira mkubwa katika Nyumba ya Malipo na Neema.
Hao ndio walio tiwa khofu na watu kwa kuwaambia: Maadui zenu wamekusanya jeshi kubwa kukupigeni, basi waogopeni. Na wao hawakudhoofika wala hawakulegea, bali walizidi Imani ya Mwenyezi Mungu na wakawa na moyo kuwa atawanusuru. Jawabu yao ikawa: Mwenyezi Mungu anatutosheleza. Yeye ndiye aliye tawala mambo yetu. Na Yeye ndiye anaye tegemezwa mambo yote.