Hebu izingitieni hali yenu ya ajabu, kuwa mnapotoka na mnakufuru baada ya Imani, na hali mnasomewa Qur'ani, na Mtume mnaye, anakubainishieni na anakukingeni na upotovu katika Dini yenu. Na mwenye kumkimbilia Mola wake Mlezi, na akashikamana na Dini yake, basi huyo amefanya vyema. Mola wake Mlezi amemwongoa kwenye Njia ya kufuzu na kufaulu.
Hakika mlango wa shari uwazi ikiwa hamumchi Mwenyezi Mungu. Basi enyi mlio amini! Mkhofuni Mwenyezi Mungu kwa khofu inayopasa, kwa kutenda anayo amrisha, na kuyaepuka anayo yakataza. Na dumuni juu ya Uislamu mpaka mtakapo kutana na Mwenyezi Mungu.
Nyote nyinyi shikamaneni na Dini ya Mwenyezi Mungu, wala msifanye jambo litalo leta mfarakano baina yenu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlivyo kuwa wakati wa ujahili nyinyi kwa nyinyi maadui. Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zenu kwa Uislamu, mkawa mnapendana, na ilhali kwa sababu ya ukafiri wenu na kufarikiana kwenu mlikuwa juu ya ukingo wa Moto, akakuokoeni kwa Uislamu. Kwa mfano wa bayana kama hii ya pekee Mwenyezi Mungu anakubainishieni daima njia za kheri, ili mdumu katika uwongofu.
Hakika njia ya kuungana kuliko kamilika juu ya Haki katika kivuli cha Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kivuli cha Mtume wake, ni kuwa muwe nyinyi Umma unao lingania (unao itia) watu waje wafuate mwendo utao waletea maslaha ya Dini na dunia, uamrishe ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, ukataze maasia. Na hapo ndipo mtakuwa mlio fuzu, kufuzu kulio kamilika.
Wala msiwe kwa kupuuza kwenu kuamrisha mema na kukataza maovu--mambo ambayo ndiyo yanayo kukusanyeni katika kheri na Dini ya Haki--kama wale walio puuza kuamrisha mema na kukataza maovu,wakagawika mapande mbali mbali, wakakhitalifiana katika Dini yao baada ya kuwafikilia hoja zilizo wazi, zenye kubainisha Haki. Na hao walio farikiana wakakhitalifiana, watapata adhabu kuu.
Adhabu kuu hiyo itakuwa Siku zitapo nawiri nyuso za Waumini kwa furaha, na kusawijika kwa masikitiko na huzuni nyuso za makafiri. Wataambiwa kwa kuwatahayarisha: Je, mmekufuru baada ya kuwa mlikulia juu ya Imani na ut'iifu wa haki, na mkaletewa hoja zilizo wazi? Basi onjeni adhabu kwa sababu ya ukafiri wenu!
Ama wale nyuso zao zimekuwa nyeupe, yaani zimenawiri, kwa kufurahi, hao watakuwa katika Pepo ambayo Mwenyezi Mungu amewapa kwa rehema yake, wadumu humo milele.
Na hizo Aya zilizo kuja za kueleza kuwa mwema na mwovu watalipwa tunakusomea, nazo zimekusanya haki na uadilifu. Na Mwenyezi Mungu hataki kumdhulumu yeyote kati ya watu na majini.