Na kuweni wa mbele katika kutenda mema ili mpate kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote, maghfira makubwa ya kufutiwa dhambi zenu, na Pepo yenye wasaa, na upana wake ni kama upana wa Mbingu zote na Ardhi. Hayo wametengenezewa wale wanao mcha Mwenyezi Mungu na wakaiogopa adhabu yake.
Hao wachamngu ndio wale wanao toa mali yao kwa kumridhi Mwenyezi Mungu wanapo kuwa na neema na wasaa, na pia wanapo kuwa na shida na dhiki na uzito, na wanazuia ghadhabu zao wanapo kasirishwa wasiwaadhibu wale wanao wakosa, bali wanawasamehe walio watendea mabaya. Hao kwa haya huhisabiwa kuwa ndio watenda mema. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwalipa mema hao watenda mema na huwa radhi nao.
Watu hao nao pindi wakifanya makosa makubwa au dhambi ndogo tu, mara humkumbuka Mwenyezi Mungu na Utukufu wake, na adhabu zake na malipo yake mema, na rehema yake na ghadhabu zake. Tena hapo hujuta kwa waliyo tenda na wakaomba msamaha wake, na hapana anaye samehe madhambi ila Mwenyezi Mungu. Na hao wachamngu hawabaki kuendelea juu ya jambo baya na ilhali wanajua ubaya wake.
Basi hao wenye kusifika kwa sifa hizi ujira wao ni maghfira makubwa kutokana na Mola wao Mlezi, Mwenye kumiliki mambo yao yote, na Bustani zipitazo mito kati ya miti yake, na humo watadumu daima. Na hayo ni malipo ya neema kubwa ilioje kwa watendao amri za Mwenyezi Mungu.
Enyi Waumini, kabla yenu shani ya Mwenyezi Mungu imewapitia kaumu zilizo kadhibisha kwa mapuuza yao. Mwenyezi Mungu akawashika kwa madhambi yao. Basi zingatieni vipi yalikuwa matokeo ya vitendo vya walio kadhibisha.
Kwa kutajwa sifa za Waumini na kueleza shani ya Mwenyezi Mungu iliyo pita kwa walio kwisha tangulia lipo Bayana na Uwongozi kwa watu wafuate njia ya kheri, na kuwaachisha njia ya shari.
Wala nyinyi msilegelege mkadhoofika katika Jihadi Fi Sabili Llahi kwa yanayo kupateni, na wala msihuzunike kwa wanao uliwa miongoni mwenu, kwani nyinyi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na Imani yenu na nguvu za Haki mnayo ipigania mko juu. Ushindi ni wenu ikiwa Imani yenu ni ya kweli, na maadamu mtadumu nayo.
Ingawa katika vita vya Uhud wameuwawa au kujuruhiwa vibaya baadhi yenu na kwa hayo mkaathirika nafsi zenu, lakini msilegee na kuhuzunika. Kwani hao makhasimu zenu yaliwapata kama hayo katika vita vya Badri. Nyakati za ushindi huendeshwa na Mwenyezi Mungu kwa watu kama apendavyo, pengine hawa hushinda, na pengine hawa, ili awatie mtihani na kuwajaribu Waumini, awateuwe wenye kusimama imara juu ya Imani yao, na apate kuwatukuza baadhi yao kwa kuwafisha mashahidi katika Sabili Llahi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi washirikina wenye kudhulumu na wangashinda kwa kusaidiwa na wengineo.