Juu ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kumiliki kila kiliomo mbinguni na ardhini na Yeye ndiye mrithi wa vyote, wamesema baadhi ya Mayahudi kwa kejeli: Mwenyezi Mungu ni fakiri, ndiyo akatutaka tutoe, na sisi ni matajiri tukitoa au tusitoe. Mwenyezi Mungu amekwisha isikia kauli yao hiyo, na ameisajili dhidi yao, kama alivyo sajili kuwauwa kwao Manabii kwa dhulma na ukhalifu na uadui. Naye atawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya Moto unao waka!
Na hiyo adhabu ni kwa dhambi zao walizo zitenda wenyewe, na malipo ya Mwenyezi Mungu hayawi ila ni kwa uadilifu, wala Yeye kabisa hawadhulumu waja wake.
Hao ndio walio sema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tusimfuate Mtume yeyote ila akileta dalili ya ukweli wake kwa kutuletea kitu cha kumkurubisha kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu, na uteremke moto kutoka mbinguni ukile hicho kitu. Ewe Nabii! Waambie: Hakika Mitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu wamekwisha kukujieni kabla yangu, wakaja na dalili zilizo wazi, na wakaja na hayo mnayo yasema. Na juu ya hayo mliwakadhibisha na mkawauwa. Kwa nini mkafanya hayo kama nyinyi ni wasema kweli katika ahadi yenu ya Imani yanapo timia mnayo yataka?
Ikiwa watakukadhibisha, Ewe Nabii, wewe usisikitike. Kabla yako wamekutangulia wengi walio kadhibishwa na watu wao kwa chuki na inda, juu ya kuwa walikuja na dalili zilizo nyooka, na Vitabu vya mbinguni vyenye kuthibitisha ukweli wa Ujumbe wao.
Hapana hivi wala hivi, kila nafsi lazima ionje Mauti. Na ikiwa hapa duniani mtapata machungu basi Siku ya Kiyama mtalipwa thawabu kwa ukamilifu. Na mwenye kuukaribia Moto akaepushwa nao basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe yenye kupita, haina dawamu.
Kuweni na yakini, enyi Waumini, kuwa mtapata mitihani na majaribio katika mali yenu, kwa kupungua, kutoa au kunyang'anywa, na katika nafsi zenu kwa Jihadi au kuuwawa au kwa maradhi na machungu. Na kadhaalika mtasikia kutokana na Mayahudi na Wakristo na mapagani, washirikina, matusi na uchokozi wa kukuudhini. Na mkiyakaabili hayo kwa kuvumilia na kumcha Mwenyezi Mungu basi itakuwa ni katika mambo mema yanayo wajibika kuazimia kuyatimiliza.