Mwenyezi Mungu ametilia mkazo kuwa Yeye ni Mmoja, na Ujumbe wake ni mmoja. Amemuamrisha Nabii wake na walio pamoja naye wasema: Tumesadiki kuwa Mwenyezi Mungu ndiye peke yake anaye faa kuabudiwa, na ndiye anaye watuma Mitume wake. Na tumeiamini Qur'ani na Sharia aliyo tuteremshia Mwenyezi Mungu, na pia tumeamini Vitabu na Sharia alizo wateremshia Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na watoto wao thinaashara, na aliyo teremsha Mwenyezi Mungu kwa Musa, nayo ni Taurati, na kwa Isa, nayo ni Injili, na walio teremshiwa Manabii wote walio baki. Hapana khitilafu katika kuamini baina ya yeyote katika wao. Na sisi kwa hivyo tumeuelekeza uso wetu kwa Mwenyezi Mungu.
Baada ya kupata utume Muhammad s.a.w. akitaka mtu Dini na sharia zisio kuwa Dini ya Islamu na Sharia yake, Mwenyezi Mungu hatamkubalia. Na malipo ya mtu huyo Siku ya Malipo ni kuwa miongoni mwa walio zikhasiri nafsi zao, ikawajibikia adhabu chungu.
Mwenyezi Mungu hakubaliani na watu walio kwisha shuhudia kuwa Mtume ni wa haki, na zikawajia dalili za kuonyesha hayo, kisha baada ya yote hayo wakamkataa, na wakakataa miujiza yake. Huo basi ni udhaalimu wao, na Mwenyezi Mungu hakubaliani na madhaalimu.
Adhabu ya watu hao wataipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama wanavyo stahiki kukasirika kwake juu yao, na laana yake, na laana ya bora ya viumbe vyake miongoni mwa Malaika na wanaadamu.
Lakini wale ambao wamejing'oa na madhambi yao, wakaingia kati ya watu wema, wakayaondoa waliyo yaharibu, basi hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafutia madhambi yao, kwani maghfira na rehema ni miongoni mwa sifa za dhati yake Tukufu.
Kukubaliwa toba na kupata rehema ya maghfira kunashurutishwa mtu adumu juu ya Imani. Wanao ipinga Haki baada ya ut'iifu na kusadiki, na wakazidisha upinzani na ufisadi na kuwaudhi Waumini, Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la hatokubali toba yao. Haiwezi kuwa toba yao hiyo ni kweli na safi na hali wanaendelea na vitendo vyao, wapo mbali na Haki na wanaigeuzia nyuso zao.
Wale wanao ipinga Haki wala hawaifuati, na wanaendelea na uwovu wao mpaka wakafa nao ni wapinzani tu, basi yeyote miongoni mwao hawezi kujitolea fidia ya kujiepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, hata ikawa anacho kitoa kuwa fidia ni dhahabu ya kujaza dunia nzima kama angeweza. Na adhabu yao ina uchungu mkali.