Enyi mlio amini! Mkiwat'ii maadui zenu makafiri, walio tangaza ukafiri wao au wakauficha, kwa hayo wanayo kuitieni kwa maneno au vitendo, watakuja kugeuzeni muingie ukafirini. Na hapo tena itakuwa mmekhasiri dunia na Akhera.
Yasikutieni unyonge yaliyo kupateni siku ya Uhud. Sisi tutaingiza khofu na vitisho katika nyoyo za maadui zenu kwa kuwa wao wamemshirikisha Mwenyezi Mungu na miungu mengine ambayo Mwenyezi Mungu hakuwateremshia hoja yoyote. Kwani Miungu hiyo hainufaishi wala haidhurishi kitu. Na makao yao yatakuwa Motoni Akhera, na maovu mno hayo makao ya madhaalimu.
Nusura ya Mwenyezi Mungu ni jambo la hakika ya kweli. Mwenyezi Mungu ametimiza miadi yake kuwa alikupeni ushindi pale mara ya kwanza mlipo wauwa maadui wengi kwa radhi yake; mpaka yalipo dhoofika maoni yenu katika vita na mkakhitalifiana kuifahamu amri ya Nabii aliyo kupeni msiondoke kwenye vituo vyenu. Baadhi yenu mkaacha vituo vyenu mlipo ona mnashinda, na wengine wakabaki mpaka mwisho. Kikundi kimoja kikaasi amri ya Mtume kikenda kuwania ngawira baada ya kwisha kuonyeshwa mkipendacho, nao ni ushindi. Mkawa makundi mawili, wanao taka raha ya dunia, na wanao taka malipo ya Akhera. Ilivyo kuwa hivyo Mwenyezi Mungu akaondoa kwenu nusura yake, mkashindwa, ili akujaribuni, atambulikane mwenye ikhlasi na asiye kuwa nayo. Lakini sasa amekusameheni kwa kuwa mmejuta. Na Mwenyezi Mungu ana fadhila kwenu kwa kukusameheni na kukubali toba yenu.
Enyi Waumini! Hebu ikumbukeni hali yenu wakati ule mlipo kuwa mkitoka mbio wala hamumsikii mtu kwa shida ya kukimbia; na Mtume anakuiteni nyuma yenu mrejee. Mwenyezi Mungu akakujazini huzuni ya kufudikiza kama wingu lilio funika nafsi zenu, ili msisikitike kwa ngawira mlizo zikosa wala kushindwa kuliko kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema makusudio yenu na vitendo vyenu.