Kisha wakatoka kwenda kwenye Jihadi na kupambana na hilo jeshi kubwa, lakini washirikina wakaingiwa na woga wakakimbia. Wakarejea Waumini kuwa wameshinda kwa neema ya salama ilhali wao wana hamu ya Jihadi, na wana malipo na thawabu na fadhila ya Mwenyezi Mungu kwao kwa vile kutia kitisho katika nyoyo za maadui zao, na wao wasipatikane na maudhi yoyote. Waliitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wao wakaistahiki fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
Mwenyezi Mungu Aliye takasika anawabainishia Waumini kwamba hao wanao kutieni khofu kuogopa kupambana na maadui zenu si lolote ila ni vibaraka wa Shetani anaye watia khofu wafwasi wake awafanye woga. Na nyinyi si katika hao. Basi msiridhie kutishwa, bali mkhofuni Mwenyezi Mungu peke yake kama nyinyi mna Imani ya kweli, na mnasimamia kutimiza yanayo lazimishwa na Imani hiyo.
Ewe Nabii! Usihuzunike ukiwaona wale ambao wanazidi ukafiri, na wanawania kuzidisha maovu. Hao hawamletei Mwenyezi Mungu madhara yoyote, kwani Yeye ni Mwenye nguvu juu ya waja wake. Bali Mwenyezi Mungu anataka wasiwe na sehemu yoyote katika thawabu za Akhera, na juu ya kukosa kwao thawabu hizo njema watapata adhabu kubwa.
Hakika watu hao walio khiari ukafiri badala ya Imani, wakatafuta ukafiri na wakaacha Imani, hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na watapata Akhera adhabu kali ya kutia uchungu mkubwa.
Wasidhani hao makafiri kuwa vile kuwapururia tunapo wakunjulia umri wao, na tukawapa njia za starehe katika maisha yao ya duniani, kuwa ndio kheri yao. Kwani kuwaongezea umri na kuwakunjulia riziki huwapelekea kudumu na kuchuma madhambi na kuzidi kustahiki adhabu ya kuwafedhehesha aliyo waandalia Mwenyezi Mungu.
Haiwi kuwa Mwenyezi Mungu akuacheni enyi jamaa Waumini katika hali mliyo nayo ya mchanganyiko wa Muumini na mnaafiki, mpaka awatenganishe baina yenu kwa misukosuko na taabu ili mumwone mnaafiki khabithi na Muumini mwema. Wala sio mwendo wa Mwenyezi Mungu kumjuulisha yeyote katika viumbe vyake khabari za ghaibu. Walakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume yake ampendaye akamjuvya anacho kitaka katika mambo yake ya ghaibu. Na nyinyi mkiamini na mkamcha Mola wenu Mlezi kwa kujilazimisha kumt'ii atakutieni katika Pepo iwe ndio malipo. Na hayo ndio malipo yaliyo bora na makubwa kabisa.
Wasidhani wanao fanya ubakhili kwa mali aliyo waneemesha Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na hawayatoi katika yaliyo waajibu na njia za kheri, kuwa ubakhili huo ni kheri yao. Bali hiyo ni shari yenye matokeo mabaya juu yao. Watalipwa malipo maovu kabisa Siku ya Kiyama, na adhabu itawaganda kama kongwa au mnyororo aliyo fungwa nayo mfungwa shingoni mwake. Kila kiumbe kinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, naye ndiye Mmiliki wao, na Yeye Aliye takasika anajua kila mnacho kitenda, na atakulipeni kwacho.