Malipo haya watayapata wale ambao nyoyo zao zimejaa Imani, na wakatangaza kwa ndimi zao wakisema kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu: Mola Mlezi wetu! Hakika sisi tumeamini kwa kuitikia wito wako. Basi tusamehe dhambi zetu, na utuhifadhi na adhabu ya Moto.
Na malipo haya huyapata wanao stahamili mashaka kwa ajili ya ut'iifu wao, na kujitenga na maasi, na kuvumilia dhiki, watu ambao ni wakweli katika kauli zao na vitendo vyao, na niya zao, wenye kudumu katika ut'iifu kwa kunyenyekea, wenye kutoa wawezacho bilhali walmali na vyenginevyo kwa sababu ya mambo ya kheri, ambao kwamba wanamtaka msamaha Mwenyezi Mungu mwishoni mwa usiku, kabla ya alfajiri, zinapo safika roho na hutengenea kuzingatia na kutafakari katika utukufu wa Muumbaji.
Mwenyezi Mungu amebainisha wazi katika maumbaji yake dalili na Ishara ambazo hawezi kuzipinga mwenye akili, ya kwamba Yeye ni Mmoja, wala hana mshirika wake, na kwamba Yeye ndiye Mwenye kusimamia mambo ya viumbe vyote kwa uadilifu. Na kwa haya pia wamekiri Malaika walio t'ahirika, na wameyajua watu wa ilimu kwa yakini, na kwamba Yeye ilio tukuka shani yake ni Mpweke katika Ungu, wala hana wa kumshinda katika jambo, na hikima yake imeenea kila kitu.
Hakika Dini ya Haki aliyo iridhi Mwenyezi Mungu ni Dini ya Tawhidi, ya Mungu Mmoja, na kumnyenyekea Yeye kwa usafi wa moyo. Mayahudi na Wakristo wamekhitalifiana na Dini hii, wakazua na wakabadilisha. Na wala kukhalifu kwao hakukuwa kwa kudanganyikiwa au kwa ujinga ilipo wajia ilimu, bali yalikuwa hayo kwa uhasidi na ushindani tu. Na mwenye kupinga Ishara za Mwenyezi Mungu, basi na angojee hisabu ya Mwenyezi Mungu, nayo yenda kasi mno.
Na hawa makafiri wakijadiliana nawe katika Dini hii baada ya wewe kuwapa hoja zote, huna haja kupigizana nao kelele kwa majadiliano. Waambie tu: Mimi na Waumini walio nifuata tumemsafia Mwenyezi Mungu peke yake ibada yetu. Na waambie Mayahudi na Wakristo na washirikina wa Kiarabu: Dalili zimekwisha bainika kwenu, basi silimuni. Wakisilimu inakuwa wameijua njia ya uwongofu na wameifuata. Na wakikataa huna lawama wewe kwa kukataa kwao. Waajibu wako ni kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu tu. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema waja wake. Hapana lolote lao, hali yao na vitendo vyao, linalo fichikana kwake.
Hakika wale wanao zipinga Ishara za Mwenyezi Mungu katika uumbaji na hizi zilizo teremka, na wakawauwa Manabii alio watuma Mwenyezi Mungu waje kuwaongoa - bila ya haki kabisa, na hiyo ni dhulma kubwa mno - na wakawauwa wale wanao waita watu wafanye haki na uadilifu, watu hao wanastahiki adhabu kali. Basi wabashirie adhabu hiyo!
Watu wenye sifa kama hizo, a'mali zao zimebat'ilika ijapo kuwa baadhi yake ni njema, na hazina matunda. Kwa hivyo haziwafai duniani, na mwisho wake ni hizaya na adhabu huko Akhera. Na wala hawana wa kuwaokoa na khasara na adhabu watayo ipata.