Fanyeni hima katika kusimamisha Swala zote na kuzidumisha. Na fanyeni hima kuwa Swala yenu iwe ni Swala bora kwa kuzitimiza nguzo zake na kumsafia niya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu katika Swala. Na timizeni ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mkumbukeni kwa usafi wa moyo na kunyenyekea Utukufu wake.
Ukikufikieni wakati wa Swala nanyi mko katika khofu basi msiache kusali, bali swalini kama muwezavyo, ikiwa huku mnakwenda kwa miguu au mmepanda kipando. Ikiondoka khofu swalini kwa kutimiza nguzo zote kama mlivyo jifunza, mkimkumbuka Mwenyezi Mungu katika Swala na mkimshukuru kwa aliyo kufunzeni, na kwa kukujaalieni kuwa katika amani.
Wanao kufa miongoni mwenu wakaacha wake zao, Mwenyezi Mungu ameusia hao wanawake wafiwa wabaki nyumbani mwa waume zao muda wa mwaka mzima kwa maliwaza na kuwaondolea ukiwa. Wala hana haki yeyote kuwatoa. Wakitoka kwa khiari yao kabla ya mwaka kwisha basi hamna dhambi nyinyi wenye madaraka mkiwaachilia wajitendee wenyewe wapendalo kwa lisio vunja Sharia tukufu. Na mt'iini Mwenyezi Mungu katika hukumu zake, na tendeni Sharia alizo kutungieni kwani Yeye ni Muweza wa kumuadhibu anaye kwenda kinyume na amri yake, na Yeye ni Mwenye hikima iliyo pita ukomo. Hakuamrishini ila lenye maslaha yenu ijapo kuwa hikima yake imepindukia ujuzi wenu.
Na wanawake walio pewa T'alaka baada ya kuingia harusi wana haki wapewe mali ya kuwaliwaza. Wapewe kwa wema, kwa kadiri ya utajiri na umasikini wa mume. Kumcha Mwenyezi Mungu kunawajibisha hayo, na pia watu wa Imani wanalazimika na hayo.
Mwenyezi Mungu anakubainishieni hukumu zake, na neema zake, na Aya zake, kwa mfano wa bayana hizi na Sharia hizi zilizo wazi zenye kuleta maslaha, ili mpate kuzingatia na mpate kutenda yaliyo kheri.
Zingatia, ewe Nabii, hichi kisa cha ajabu, na ukijue! Hao watu walitoka wakaacha majumba yao ati wanakimbia Jihadi kwa kuogopa kufa, na hali wao ni maelfu kwa maelfu. Mwenyezi Mungu akawahukumia kifo na udhalili kutokana na maadui zao. Walipo bakia walio bakia wakasimama kupigana Jihadi, Mwenyezi Mungu aliwapa uhai kwa kuwapa nguvu. Hakika uhai huu wenye nguvu ulio kuwa baada ya madhila umekuja kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu, na unastahiki shukrani. Lakini wengi wa watu hawashukuru.
Mlivyo jua kuwa hamwezi kuyaepuka mauti kwa kuyakimbia, basi piganeni Jihadi, na zitumieni nafsi zenu kwa kulitukuza Neno la Mwenyezi Mungu, na kuweni na yakini kuwa Mwenyezi Mungu anayasikia wanayo yasema woga na wanaafiki wanao kimbia, na wayasemayo Mujaahidina wanao pigana, na anayajua anayo dhamiria kila mtu katika nafsi yake. Na kwa lilio kheri atamlipa kheri, na kwa shari atamlipa shari.
Na Jihadi kwa Njia ya Mwenyezi inhaitaji mali, basi toeni mali yenu. Mtu gani huyo ambaye hatoi mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa radhi ya nafsi yake, na hali Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa atamrejeshea mara nyingi sana zaidi? Na riziki zote zimo katika mkono wa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye humkunjia amtakaye na akamkunjulia amtakaye kwa yaliyo na maslaha yenu. Marejeo ni kwake Yeye, naye atakulipeni kwa mujibu mlivyo toa. Na ilivyo kuwa riziki zote ni kwa fadhila ya Mwenyezi na Yeye ndiye mwenye kutoa na mwenye kunyima basi ameitwa yule mwenye kutoa kuwa ni kama mkopeshaji ili kuhimiza na kupendekeza kutoa, na kutilia mkazo kuwa malipo ni mara nyingi sana duniani na Akhera.