Wapotovu walio acha njia ya uwongofu wamezoea kuyashika waliyo yarithi kwa baba zao katika itikadi na vitendo. Wanapo itwa wafuate uwongofu wa Mwenyezi Mungu husema: Hatuachi tuliyo yakuta kwa baba zetu. Katika ujinga mkubwa kabisa ni kukhiari kufuata wazee kuliko kumt'ii Mwenyezi Mungu na kufuata uwongofu wake. Kefu basi inapo kuwa baba zao hawanacho wakijuacho katika Dini, na hawana mwangaza wa kuwanawirisha uwongofu na Imani?
Na mfano wa kuwaita hao makafiri wanao pinga haki na uwongofu na wasiitikie wala wasifahamu wanaitiwa nini ni mfano wa mchunga kondoo anapo wasemeza hayawani. Hawafahamu kitu wala hawasikii ila sauti, wala hawaelewi kinginecho. Basi hao kadhaalika kwa mintarafu ya Haki ni viziwi wa kusikia, vipofu wa kuona, mabubu wa kusema. Hawatamki jema, wala hawatoi la akili.
Na Sisi tumewaruhusu watu kula kila kilicho halali tulicho waumbia katika ardhi. Na tumewakataza wasifuate nyayo za Shetani. Wakifanya hivyo watakuwa wameongokewa, lakini wakikataa basi Sisi tunawakhusisha Waumini tu kwa uwongofu wetu, na tunawabainishia wao kilicho halali na haramu. Basi enyi Waumini! Mmeruhusiwa kula kila chakula kitamu kilicho chema, sio kichafu. Basi mshukuruni Mwenyezi Mungu aliye kuwekeeni wazi neema ya kumakinika kwa vitu vizuri na kukuhalalishieni, na kwa neema ya ut'iifu na kufuata amri yake ili ibada zenu zitimie. Qurani imeutangulia utibabu wa kisasa kwa kukataza kula mzoga, kwani kifacho kwa ukongwe au ugonjwa husabibishwa na sumu inayo mdhuru mlaji. Kadhaalika cha kunyongwa au maradhi huinajisi damu, na ndani yake huwamo vingi vya kudhuru kama jasho na mkojo. Na nguruwe husabibisha maradhi ya khatari kama TRICHINOSIS ambayo khatimaye huharibu moyo na mapafu na husabibisha mauti.
Sio yaliyo harimishwa wanayo zua Washirikina na Mayahudi. Lakini mlicho harimishiwa nyinyi Waumini ni nyamafu, mzoga, yaani mnyama asiye chinjwa, na mfano wake katika kuharimishwa ni nyama ya nguruwe, na nyama ambaye wakati wa kuchinjwa ametajiwa jina lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu, kama vile miungu ya uwongo au mfano wake. Juu ya hivyo mtu akilazimika kwa dharura kula kidogo katika vilivyo katazwa kwa ajili ya njaa, na hakupata kinginecho, au kwa kulazimishwa, basi hana makosa juu yake. Lakini ajitenge na mwendo wa kijaahili, kutaka kula vilivyo katazwa kwa kutamani tu, na wala asipite kiasi kula kuliko cha kuondoa njaa tu. Hali ya dharura inaruhusisha kinacho harimishwa, kwa sababu mauti ya yakini yanashinda madhara yanayo weza kustahamilika, na kwamba mwenye kulazimika kwa dharura haimfalii kupindukia mpaka wa dharura, wala asikiuke kile alicho lazimika kukila.
Miongoni mwa watu wanao jua aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu kipo kikundi kinacho ficha baadhi ya maandishi ya ufunuo kwa ajili ya sababu fulani za kilimwengu. Mayahudi, mathalan, wakificha mengi yaliyo kuja katika Taurati ya kueleza sifa za Mtume kwa kukhofu wasije wakasilimu watu wa mila yao na kwa hivyo utukufu wao ukaondoka na wakapoteza mapato yao na vyakula vyao vitamu. Na hakika chakula chao wakilacho kwa njia hii ni kama kula moto, kwani hayo yatawapelekea kuingia Motoni. Mwenyezi Mungu atawatupilia mbali Siku ya Kiyama, wala hatawasafisha uchafu wao, na mbele yao kuna adhabu ya kuumiza kweli.
Hao ndio wenye madhambi walio khiari upotovu wakaacha uwongofu, na kwa hivyo wakastahiki adhabu ya Akhera badala ya kupata msamaha. Watakuwa kama mwenye kununua baat'ili kwa haki, na chenye upotovu kwa chenye uwongofu. Hakika hali yao ni ya kustaajabisha, kwa kuwa wanavumilia kufanya mambo ambayo hayana budi kuwapelekea kwenye adhabu, na tena wakawa wenyewe wakayaonea uzuri hayo yanayo wapeleka huko!
Nao yamewapasa malipo waliyo kadiriwa kwa kukikataa Kitabu cha Mwenyezi Mungu alicho kiteremsha kwa haki na kweli. Na wamekhitalifiana kwacho khitilafu kubwa iliyo wapelekea kupenda kujadiliana na kujitenga na Haki, na kufuata pumbao, wakakigeuza na kukifisidi na kukifasiri kinyume na maana yake ya hakika.