Na Hija inakuwa katika miezi mnayo ijua, kwani jambo hili ni maarufu kwenu tangu zama za Ibrahim a.s. nayo ni miezi ya Mfungo Mosi, Mfungo Pili na Mfungo Tatu. Mwenye kuazimia faridha ya Hija katika miezi hii na akaingia basi afuate vilivyo adabu zake. Katika adabu za Hija ni kuwa mwenye kuharimia ajiepushe na kuingiana na wakeze, na kufanya maasi ya kutukanana na mengineyo, kujadiliana na kubishana na Mahujaji wenziwe, na ajiepushe na kila linalo pelekea chuki na khasama ili atoke katika Ihramu yake naye hali ana hishima yake. Ajitahidi kufanya kheri na kutafuta malipwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua hayo na ni Mwenye kulipa vitendo vyema. Na mchukue zawadi za Akhera yenu kwa kuchamngu na kufuata amri za Mwenyezi Mungu na kuyaepuka ayakatazayo. Hiyo, basi ndio zawadi bora. Na kuweni wenye kuhisi khofu ya Mwenyezi Mungu katika yote mnayo yafanya na mnayo yawacha kwa mujibu wa akili na hikima njema. Katika vitendo vyenu vyote msichanganyishe hata chembe na mambo ya pumbao au makusudio ya kidunia.
Na walikuwako miongoni mwenu ambao wakiona vibaya kufanya biashara na kutafuta riziki wakati wa msimu wa Hija. Basi mnaambiwa kuwa hapana ubaya kwenu hayo, bali mnaweza kuchuma maisha kwa njia ziliyo ruhusiwa na sharia, na mtafute fadhila na neema za Mwenyezi Mungu. Wakitoka Mahujaji A'rafat baada ya kusimama huko, na wakafika Muzdalifa katika mkesha wa Idi ya Kuchinja, wamtaje Mwenyezi Mungu hapo Masha'ril Haram, napo ndipo kwenye kilima cha Muzdalifa, kwa kusoma Tahlili na kuitikia Labbaika na kusoma Takbir. Na wamtukuze Mwenyezi Mungu wakimhimidi na kumshukuru kwa vile alivyo waongoa kwenye Dini ya Haki na ibada iliyo nyooka katika Hija na Umra, na ilhali kabla ya hapo walikuwa katika walio potea njia ya uwongofu.
Makureshi walikuwa hawasimami na watu wengine katika A'rafat juu ya kuwa wakijua kuwa baba yao Ibrahim akisimama hapo. Na hayo ni kwa kujitukuza wasiwe sawa na wengineo na hali wao ati ni watu wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu na ni wakaazi wa katika pahala patakatifu. Wakidai kuwa hayo ni kuitukuza Makka wasitoke kwenda A'rafat ambako si kutakatifu kama Makka. Mwenyezi Mungu akawalazimisha wazing'olee mbali hizo ada za kijinga, na wasimame katika A'rafat, na watoke huko kama watokavyo watu wote. Kwani hapana yeyote aliye bora kuliko mwengine katika utendaji wa ibada. Na inawapasa wamwombe Mwenyezi Mungu maghfira katika mwahala humu mwenye baraka. Hayo ndiyo yana maelekeo zaidi Mwenyezi Mungu kuwasamehe dhambi na makosa yao, na akawarehemu kwa fadhila yake.
Mkisha maliza a'mali za Hija na ibada zake wacheni mliyo kuwa mkiyafanya zama za ujahili ya kutafakhari kwa baba zenu na kukumbusha mambo yao, bali makumbusho yenu na kutukuza kwenu kuwe kwa Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa mkiwakumbuka baba zenu, bali mtajeni Yeye kwa wingi zaidi kuliko wazee wenu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuzitawala neema zenu na neema za baba zenu vile vile. Na humu mwahali mwa Hija ndio khasa mwahala mwa dua na kuombea fadhila na kheri na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu. Na walikuwako baadhi ya Mahujaji wakifupiza dua zao kwa mambo na kheri za dunia tu. Hao hawapati sehemu yoyote ya Akhera.
Na wapo watu ambao Mwenyezi Mungu amewawezesha nyoyo zao zikapelekea kuomba kheri ya dunia na Akhera, na wakamwomba Mwenyezi Mungu awaepushe na shari na adhabu ya Moto.
Hawa wanapewa kama walivyo jaaliwa kuyachuma kwa kumwomba na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu humlipa kila mtu kama anavyo stahiki, na ni Mwepesi wa kuhisabu na kulipa.