Miongoni mwenu enyi wanaume, akitokea aliye kufa akaacha mke asiye na mimba, basi mwanamke yampasa akae eda, yaani asiolewe, muda wa miezi mine ya kuandama na siku kumi mchana na usiku, ili kuhakikisha kiliomo tumboni, kama ana mimba au la. Ukisha muda huu, enyi wazee, hapana ubaya kwenu mkiwaachilia kuleta mtu wa hishima kuja mposa. Haifai nyinyi kuwazuilia hayo, na haijuzu kwao kufanya mambo yanayo kataliwa na Sharia, kwani Mwenyezi Mungu anajua vyema siri zenu na anavijua vitendo vyenu, na atakuhisabuni kwa myatendayo.
Katika muda wa eda hapana dhambi kwenu, nyinyi wanaume, mkiwaonyesha dalili kuwa mnadhamiria kutaka kuwaoa waliomo edani kwa kufiwa na waume zao, lakini hayo yawe ni kudhamiria ndani ya moyo tu. Mwenyezi Mungu hakika anajua kuwa hamwezi kuacha kuwazungumza waliomo edani, kwani ni maumbile baina ya wanaume na wanawake. Kwa hivyo mmepewa ruhusa kuashiria bila ya kubainisha kwa maneno. Basi msiwape ahadi ya kuwaoa ila iwe ishara isiyo ovu wala ya uchafu. Basi msifunge ndoa mpaka baada ya kwisha eda. Na kuweni yakini kuwa Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha ndani ya nyoyo zenu. Basi iogopeni adhabu yake, wala msitende anayo kukatazeni. Wala msikate tamaa na rehema yake pale mnapo ikhalifu amri yake, kwani Yeye ni Mwenye kughufiria mno, na anakubali toba ya waja wake, na anasamehe makosa, kama alivyo Mpole hafanyi haraka ya kuwaadhibu wale wanao vunja aliyo yakataza.
Wala hapana dhambi kwenu enyi waume, wala hapana mahari juu yenu mkiwaacha wake kabla ya kuingia harusi na kabla hamjawatajia kiasi cha mahari. Lakini wapeni zawadi kama kuwapoza kuwapunguzia machungu ya moyo. Na hicho mnacho toa kiwe cha kuridhisha na kupendeza moyo. Tajiri atoe kwa kadiri ya wasaa wake, na fakiri kwa kadiri ya hali yake. Na zawadi hiyo ni katika a'mali za kheri wanazo jilazimisha nazo watu wenye muruwa na watu wa kheri na ihsani.
Pindi mkiwapa T'alaka wanawake kabla ya kuingia harusi lakini baada ya kwisha wafikiana mahari, basi ni haki yao hao wat'alaka wapewe nusu ya mahari, ila wenyewe kwa ridhaa yao wakikataa kuchukua kitu. Na wao pia hawapewi zaidi ya nusu ila waume nafsi zao wakasamehe na wakatoa mahari yote kaamili. Na kila mmoja wapo kusamehe ndio ubora zaidi na ni kumridhisha zaidi Mwenyezi Mungu, na ndio mambo yanavyo elekea kwa wachao Mungu. Basi msiache huu mwendo wa kusameheana. Na kumbukeni kuwa kheri iko katika kufadhiliana na kufanyiana ihsani. Hayo ndiyo yanayo pelekea kupendana baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema dhamiri zenu na atakulipeni kwa fadhila mzitendazo.