Na wao hakika waliyasadiki waliyo yazua mashetani wao na wapotovu wao juu ya ufalme wa Suleiman, walipo dai kuwa Suleiman hakuwa Nabii wala si Mtume aliye teremshiwa ufunuo (Wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bali alikuwa ni mchawi tu anaye tegemea msaada wa uchawi wake. Na kwamba ni uchawi wake huu ndio ulio mjengea ufalme wake na ukamwezesha aweze kuwatawala majini, na ndege, na upepo. Kwa hivyo walimsingizia ukafiri Suleiman, na hali Suleiman hakukufuru, lakini hao mashetani waovu ndio walio kufuru. Wao ndio walio zua uzushi huu, wakaingia kuwafunza watu uchawi wao na walio pokea katika mabaki yaliyo teremka katika Baabil (Babilonia) kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta. Na hawa Malaika wawili hawakuwa wakimfundisha mtu yeyote mpaka wamwambie: Sisi ni mtihani uwe ni majaribio kwenu, tunakufundisha mafunzo ambayo yanaweza kuleta fitna na ukafiri, basi jifunze lakini tahadhari usiitumie ilimu hii. Na lakini watu hawakunasihika kwa nasiha hii, na wakatumia hayo waliyo jifunza kwa hao Malaika wawili ya kumgombanisha mtu na mkewe. Naam, hawa mashetani waovu wamekufuru walipo zua katika uzushi wao na hadithi zao za uwongo wakafanya hayo ndio wasila na udhuru wa kuwafundishia Mayahudi uchawi. Na wao hao wachawi hawawezi kumdhuru yeyote, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Yeye anayeweza kumletea mtu madhara pindi akipenda. Na hayo ya uchawi wao yanawadhuru hao wanao jifunza katika dini yao na dunia yao, na wala hawapati faida yoyote. Na wao wanajua kweli ya kujua ya kwamba anaye elekea upande huu hana sehemu yoyote katika neema za Akhera. Na kama wamebakia na ujuzi wowote yafaa wajue kuwa haya waliyo yakhiari kwa ajili ya nafsi zao ni hadi ya kuwa maovu.
Na lau kuwa wao wameiamini Haki na wakauogopa ufalme na uwezo wa Mola wao Mlezi, basi Mwenyezi Mungu angeli walipa malipo mema, na hayo bila ya shaka yoyote yangeli kuwa ni bora zaidi kuliko wanayo yapata katika hadithi zao za uwongo na dhamiri zao mbovu wanazo zidhamiria, lau kuwa wanabagua linalo kuwa na manufaa wakaacha lenye madhara.
Enyi mlio amini! Tahadharini na hawa Mayahudi. Msimwambie Mtume pale anapo kusomeeni ufunuo: "Raa'ina" kwa kukusudia akuwekeni pahala pa uangalizi wake, yaani (Tuchunge, Turai), na akupeni muda katika kusoma kwake mpaka mzingatie na mhifadhi. Kwani watu makhabithi miongoni mwa Mayahudi husaidiana kutaka kukuigeni na kupindua ndimi zao kwa neno hilo mpaka likawa neno la matusi wanalo lijua wao. Na wao humkabili Mtume kwa neno hilo kwa kumfanyia maskhara. Lakini nyinyi tumieni neno jingine wasilo weza Mayahudi kulipatia njia ya kufanya ukhabithi wao na maskhara yao. Tumieni neno: "Ndhurna" yaani "Tuangalie". Na sikilizeni vyema anayo kusomeeni Mtume. Na Mwenyezi Mungu anawadundulizia adhabu kali kwa Siku ya Kiyama hawa wanao mfanyia maskhara Mtume. Katika lugha ya Kiyahudi ya Kiebrania lipo neno "Rai'nu" ambalo limejengwa na neno "Ra'" kwa maana ya "Shari" na neno "nu" linaonesha jamii, wingi. Na maana ya neno lote ni kuwa "Wewe ni shari yetu", wakikusudia kumwambia Mtume hayo.
Na yafaa mjue kuwa hawa makafiri wa Kiyahudi na washirikina waabuduo masanamu hawakutakieni ila mdhurike tu, wala hawapendelei iteremke kheri yoyote kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu hathamini chochote wanacho kipenda wala wanacho kichukia. Kwani Mwenyezi Mungu humteua amtakaye kwa kumkhusisha kumpa rehema yake, na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.