Nao walikutaka wewe Muhammad, uwaletee miujiza, ishara, ile waliokuja nayo Musa na Manabii wa Wana wa Israili. Sisi yatutosha kuwa tumekutia nguvu kwa kukuletea Qur'ani. Na Sisi tunapo acha nguvu kumpa Nabii anaye kuja nyuma kwa muujiza wa Nabii aliye tangulia, au tukawasahaulisha watu athari za muujiza ule, basi Sisi humletea huyu Nabii aliyekuja baadaye muujiza, kuwa ni Ishara, au Aya, iliyo bora zaidi au mfano wa ile ili kuwa ni dalili ya ukweli wake. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. (Na hapana Ishara, Muujiza au Aya, iliyo kubwa na bora na yenye kudumu kuliko hii Qur'ani.)
Na Yeye, Mwenyezi Mungu, ndiye mwenye ufalme wa Mbingu na Ardhi katika mikono yake. Na nyinyi watu hamna mlinzi wa kukusaidieni, wala tegemeo la kukunusuruni isipokuwa Yeye.
Na kwa kule kumtaka kwenu Mtume wenu Muhammad miujiza fulani pengine ilikuwa mnawaiga Wana wa Israili wa zama za Musa, walipo mtaka awaletee miujiza maalumu. Kutaka kwenu huku kunaficha nyuma yake inda na kumili kwenye ukafiri, kama kulivyo kuwa kule kutaka kwa Wana wa Israili kumtaka Mtume wao. Na mwenye kufuata nyayo za inda na ukafiri akaacha usafi wa kutaka Haki na Imani basi huyo ameipotea Njia iliyo sawa iliyo nyooka.
Na wengi miongoni mwa Mayahudi wametamani kukurejesheni, enyi Waislamu, kwenye ukafiri baada ya kuwa nyinyi mmekwisha amini. Na haya juu ya kuwa wao imekwisha wadhihirikia kutoka na hicho hicho Kitabu chao kuwa nyinyi mpo juu ya Haki. Na hayakuwa hayo ila ni kuwa wanakuhusuduni na wanaogopa utawala usiwatoke mikononi mwao mkapewa nyinyi. Basi nyinyi wapuuzeni, na wasameheni, na waachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu akuonyesheni lipi jengine la kuwafanyia, kwani Yeye ni Muweza wa kukupeni ushindi juu yao, na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Na hifadhini mambo ya Dini yenu: Shikeni Swala, toeni Zaka, na vitendo vyote vyema mnavyo fanya kujitangulizia nafsi zenu, na sadaka mnazo toa, malipo yake mtayakuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua vyema myatendayo; ujuzi wake ni ujuzi wa mwenye kutazama akaona.
Na katika upotovu wa Mayahudi na Wakristo na matamanio yao ya uwongo, ni yale madai yao kila mmoja wao kuwa hataingia Peponi ila mwenye kufuata dini yao. Hebu watakeni wa kutoleeni ushahidi wa hayo madai yao kama kweli wanasema kweli.
Na wala hawatapata ushahidi wa hilo. Kwani kweli ilivyo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaandalia neema za Pepo, na atawalipa malipo Siku ya Kiyama, na atawalinda na khofu na huzuni, hao ambao wanao msafia niya Mwenyezi Mungu na wanafuata Haki, na vitendo wavitendavyo ni vyema.