Enyi Watu wa Kitabu! Msipindukie haki, mkazidisha kupita kiasi katika dini yenu, wala msimzulie uwongo Mwenyezi Mungu, mkaukanya utume wa Isa, au mkamfanya kuwa ni Mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Kwani Masihi ni Mtume kama walivyo Mitume wengine. Mwenyezi Mungu amemuumba kwa uwezo wake na neno lake alilo mbashiria kwalo, na Jibrili akampulizia Maryamu roho ya Mwenyezi Mungu. Hii ni siri katika siri za uwezo wake Mwenyezi Mungu. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wote imani ya kweli. Wala msidai kuwa katika Ungu kuna Utatu!! Tokeni katika upotovu huu, itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu, wala hana mshirika wake. Naye ametakasika na kuwa na mwana! Na kila kilioko katika mbingu na ardhi ni chake. Na Yeye Mwenyewe anajitosha peke yake kuwa ni Mwendeshaji wa Ufalme wake. (Kuitwa Nabii Isa Neno au Roho iliyo toka kwa Mungu, hakumpi Ungu. Yeye ni neno kwa kuumbwa kwa amri ya "Kun", "Kuwa" akawa. Haya ni kuwapinga Mayahudi walio dai kuwa yeye ni mwanaharamu. Basi wanaambiwa kuwa ameumbwa kama vilivyo umbwa vitu vyote, kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Naye ni Roho iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu kama walivyo pewa Waumini wote (58.22) na alivyo puliziwa Adam (15.29) na kwa hivyo wanaadamu wote (32.7-9). Hapana hata pahala pamoja katika Injili ziliomo katika Biblia ambapo Yesu (Nabii Isa a.s.) alijiita mwenyewe Mwana wa Mungu. Kila mara akijiita Mwana wa Adamu. Na alipo mwita Mungu Baba, alikusudia ni Baba wa watu wote, kama alipo sema: "Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu." Injili ya Yohana 10.33-36.)
Masihi hakujiona bora hata akatae kuwa ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala hawakujiona bora Malaika walio karibishwa. Na mwenye kutakabari na kujiona mtu wa juu hataweza kuikimbia adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku atakayo wakusanya watu kwa ajili ya hisabu.
Ama walio amini wakatenda mema atawalipa thawabu za vitendo vyao, na atawazidishia kwa fadhila yake, kwa kuwakirimu na kuwaneemesha. Na ama wale walio kataa kumuabudu, na wakajiona bora wasimshukuru, hao amewaandalia adhabu yenye machungu makali. Hapana msaidizi wa kuwakinga nayo wala wa kuwanusuru.
Enyi watu wote! Zimekwisha kujieni dalili zilizo wazi za ukweli wa Mtume Muhammad. Na tumekuteremshieni kwa ulimi wake Qur'ani iliyo wazi kama mwangaza, unao angaza Njia, na inayo kuongozeni kwendea mafanikio.
Ama walio msadiki Mwenyezi Mungu na ujumbe wake alio leta, na wakaifuata Dini yake, atawatia katika Bustani zake Akhera, na atawamiminia rehema yake, na atawakusanya katika ukunjufu wa fadhila yake, na atawawezesha hapa duniani kuthibiti katika Njia yake Iliyo Nyooka.