Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu ila Yeye, wala hapana mwenye uweza ila Yeye, hapana shaka atakufufueni baada ya kufa kwenu, na atakukusanyeni kwenye kituo cha kuhisabiwa kwa ajili ya malipo. Hayo hayana shaka. Yeye anasema hayo, basi msiyatilie shaka maneno yake. Na kauli gani iliyo ya kweli zaidi kuliko kauli ya Mwenyezi Mungu?
Haikufaliini, enyi Waumini, kukhitalifiana katika mas-ala yaliyo khusu wanaafiki, ambao wanadhihirisha Uislamu na wanaficha ukafiri. Haikufaliini kukhitalifiana kwa mas-ala yao, kuwa ati wao ni Waumini au makafiri? Wauwawe au waachiliwe? Je, wameelekea kuongoka au hawatarajiwi uwongofu? Fahamu zao zimegeuzwa kwa yaliyo chumwa na vitendo vyao. Shari imekuwa ndio inayo wahukumu, basi usimtarajie kuongoka yule ambaye Mwenyezi Mungu kwa ujuzi wake wa tangu na tangu kesha mkadiria asiongoke. Kwani aliye andikwa katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu wa tangu azali kuwa ni mwenye kupotea basi huna njia ya kumwongoa.
Hakika nyinyi mnapenda kuwaongoa hawa wanaafiki, na wao wanapenda nyinyi mkufuru kama wao, ili muwe nyote sawa kwa ukafiri. Ilivyo kuwa hivyo basi msitake wa kukuungeni mkono miongoni mwao. Wala msiwafanye wenzenu, mpaka wakubali kutoka huko kwao kuwania Jihadi kwa ajili ya Uislamu. Hivyo tu ndio itawatoka sifa ya unaafiki. Lakini wakiyakataa hayo, wakaungana na maadui zenu, basi wauweni popote mtapo wapata, wala msiwaone kuwa ni wenzenu, wala msiwachukulie kuwa ndio wasaidizi wenu.
Katika wanaafiki, wanao stahiki kuuliwa kwa fisadi yao kuwafisidi umma wa Waumini, watoe wale ambao wamefungamana na kaumu ambao baina yao na Waumini yapo mapatano ya kuzuia kuuliwa aliye fungamana na upande mmoja wapo. Au vile vile ambao wametatizwa hawajui wapigane pamoja na watu wao, ambao ni maadui wa Waislamu wasio na mkataba nao, au wapigane pamoja na Waumini? Kwani hakika wale wa kwanza inakatazwa kuwauwa kwa ajili ya mkataba, na wengine inakatazwa kuwauwa kwa kuwa hawajui moja wapo la kutenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amependa angeli wajaalia hao wakupigeni vita. Ilivyo kuwa wamekhiari kukaa tu wasikupigeni na wakaingiana nanyi kwa salama na amani, basi haikufaliini nyinyi kuwauwa. Hapana ruhusa kufanya hayo.
Mkiwashinda washirikina, hao wanaafiki huwa pamoja nanyi; na washirikina wakiwashinda Waislamu, wao huwa pamoja na washirikina. Wao hutaka wapate amani kwa Waislamu na wapate amani kwa jamaa zao washirikina. Hawa wamo katika upotovu na unaafiki wa moja kwa moja. Ikiwa hawatoacha kukupigeni vita na wakakutangazieni amani na salama, basi wauweni popote muwapatapo. Kwani kwa kuto kujitenga na kukupigeni vita, basi inakuwa Waumini wana haki kuwauwa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa Waumini hoja iliyo wazi kuwapiga vita.