Mwenyezi Mungu anawakataza waja wake wasiseme maneno maovu, ila yule aliye patwa na dhulma. Ni halali kwake kumshitaki aliye mdhulumu, na autaje uovu aliyo tendewa. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kusikia vyema maneno ya aliye dhulumiwa. Na ni Mjuzi wa dhulma ya mwenye kudhulumu. Na atamlipa kwa kitendo chake hicho.
Mkiyadhihirisha mema myatendayo, au mkayaficha, au mkamsamehe anaye kufanyieni uovu, Mwenyezi Mungu atakulipeni kwa kufuata khulka yake Mtukufu, ya kusamehe na hali ana uwezo kaamili. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni mwingi mno wa kusamehe, Mwenye kukamilika uwezo wake.
Hakika wasio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanao taka kufanya ubaguzi katika imani ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanasema: Tunawaamini baadhi ya Mitume, sio wote, hao wanawaamini wawapendao na wanawakataa wasio wapenda. Na lilio waajibu ni kuwaamini wote, kwani Imani haikubali kukatwa mapande mapande.
Hawa wote ndio walio ungama ukafiri wao ulio wazi. Na Mwenyezi Mungu amekwisha waahidi wao na mifano ya hao adhabu kali yenye kudhalilisha.
Na ama wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala hawakumkanusha hata mmoja wapo kati yao, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atawalipa malipo makubwa kwa ajili ya Imani yao iliyo kamilika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira kwa wenye kutubu, na ni Mwenye kuwarehemu waja wake.
Ewe Mtume! Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi wapendao kuudhi, wanakutaka ulete dalili ya ukweli wa unabii wako. Uwaletee kitabu makhsusi kiwateremkie kutoka mbinguni kithibitishe ukweli wa utume wako, na kiwatake wakuamini na kukut'ii! Ukiyaona makuu hayo wayatakayo, wewe usifanye haraka. Kwani wenzao walio tangulia walifanya kero vile vile, wakamtaka Musa makubwa kuliko hayo. Walimwambia: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu tumwone kwa macho. Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa lile kero lao na dhulma yao kwa kuwapiga radi iliyo wateketeza!! Kisha watajie hawa watu kosa kubwa zaidi na ovu zaidi, nalo ni pale walipo mfanya ndama kuwa ni Mungu wao, wakamwacha Mwenyezi Mungu aliye waumba. Haya baada ya kwisha ona dalili zote alizo zionyesha Musa kwa Firauni na kaumu yake!! Kisha juu ya hayo Mwenyezi Mungu akawakunjulia usamehevu wake kwao, na Mwenyezi Mungu akampa nguvu Musa kwa hoja zilio wazi, na neno madhubuti.
Mwenyezi Mungu akaunyanyua mlima juu ya Wana wa Israili ili kuwatisha kwa kule kuikataa kwao sharia ya Taurati, mpaka wakaikubali. Akachukua kwao agano, na akawaamrisha waingie mjini hali wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Wala wasiyakiuke aliyo waamrisha kushika ibada katika siku ya Sabato, yaani Jumaamosi.(Imeitwa "Sabt" Kiarabu, "Shabbath" Kiyahudi, "Sabbath" Kiingereza, na "Sabato" Kiswahili, maana yake "Mapumziko" kwa kuwa ni siku ya mapumziko kwa Mayahudi.) Na Mwenyezi Mungu alichukua kwao ahadi ya nguvu.