Hakika wale wanao kaa wakipanga mambo yao kisirisiri, mambo hayo hayana kheri, kwa sababu shari ndio huchipuka katika ufichoni. Lakini ikiwa mazungumzo hayo ni kwa jambo la sadaka ya kuwapa watu, au kufanya jambo lolote lisio baya, au kupanga mipango ya kusuluhisha baina ya watu, hayo si mabaya. Kwani hayo ni mambo ya kheri. Na mwenye kufanya hivyo kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataa'la, basi Mwenyezi Mungu atampa malipo makubwa duniani na Akhera.
Na anaye mpinga Mtume s.a.w. baada ya kwisha itambua Njia ya Haki na Uwongofu, na akaifuata njia isiyo kuwa ya Waumini, na akaingia kwenye urafiki na maadui wa Waumini, basi huyo atakuwa na hao. Kwani amekhiari kuwa hao ndio wawe marafiki zake na walinzi wake. Mwenyezi Mungu atakuja mtia Motoni Siku ya Kiyama.
Hakika mwisho huu wa kuumiza ni wao hao vile vile, kwani hao ni maadui wa Uislamu. Mfano wake ni mfano wa mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Hakika kila dhambi yaweza kughufiriwa, ila kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na kumuabudu mwenginewe asiye kuwa Yeye, na kumpinga Mtume katika Haki. Ni shani ya Mwenyezi Mungu kusamehe madhambi, ila dhambi ya kumshirikisha Yeye katika ibada. Kwa jenginelo lisilo kuwa hili Yeye humsamehe amtakaye. Anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada na kumtegemea, basi huyo ameipotea Haki, na amekuwa mbali nayo mno; kwani mtu huyo ameifisidi akili yake na nafsi yake pia.
Katika upotovu ulio wazi kabisa ambao uko mbali na Haki ni ule wa mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Huyo anaabudu kitu ambacho hakisikii wala hakioni, hakidhuru wala hakinafiishi. Na huita hiyo miungu yake kwa majina ya kike, kama Laata na Uzza na Manaata na mengineyo ya majina ya kike. Yeye hakika kwa hivyo anamuabudu Shetani.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekwisha mfukuza huyu Shetani kutokana na kivuli cha rehema yake, na amemjaalia awe katika njia ya upotovu. Na Shetani ameapa, na amejichukulia ahadi mwenyewe, kuwa atachota miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu idadi maalumu awapumbaze kwa upotovu wake na awatie wasiwasi kwa shari yake.
Hakika kiapo chake Shetani ni kuwa atawapoteza wale anao wapumbaza kwa kuwatenga mbali na Haki, na kuchochea pumbao lao na matamanio yao, mpaka wakawa wamepotea wanatanga tanga katika mawazo na tamaa za uwongo. Wakisha kuwa katika kuzainiwa huku na tamaa hizo chini ya utawala wake Shetani, tena huwatokomeza kwenye mambo yasiyo ingia akilini, na huwapelekea hao wafikiri kufanya hayo ni ibada. Na ilhali haya yote ni mawazo ya uwongo tu. Basi huwatia wasiwasi wakatenda mambo, kama kwa mfano kuwakata masikio baadhi ya ngamia wao, wageuze khulka aliyo iumba Mwenyezi Mungu. Wakafanya kuwa ngamia aliye katwa masikio yake hachinjwi, wala hafanyishwi kazi, wala hazuiliwi kwenda machungani atakavyo. Yote haya ni kwa amri yake Shetani kuwazaini. Tena huwatia wasiwasi mpaka wakaona kuwa hayo ni katika dini. Na hakika wao inakuwa wanamfuata yeye Shetani, na wanamfanya yeye ndiye wa kuwanusuru, na ndiye wa kumfuata badala ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shetani ndiye msaidizi wake wa kumfuata, basi amekhasiri khasara kubwa iliyo wazi. Kwani hapo anakuwa amepotea njia ya Haki, na ameipumbaza akili yake, na utampata ufisadi duniani, na adhabu Akhera.
Shetani huwapambia shari, wakaiona nzuri, na huwaahidi manufaa watayo pata pindi wakitenda kitendo fulani, na huwatia katika nafsi zao matumaini ya kuyatumai. Na hapana lolote analo waahidi na analo wapambia ila ni udanganyifu mtupu.
Hakika hao walio zipoteza akili zao na wakafuata wasiwasi wa Shetani anao watia katika nafsi zao, mwisho wao ni kuendea Jahannamu, wala hawatapata njia ya kutoka huko.