Ewe Nabii Muaminifu, ukiwa nao na Swala ya Jamaa inasaliwa, msisahau kutahadhari na maadui. Na hayo ni kuwagawa Waislamu makundi mawili. Moja lianze kuswali kwa kukufuata wewe, na wakati huo la pili lisimame kwa hadhari na silaha likilinda vifaa. Ukisha nusu ya Swala, kundi lilio sali nawe lende nyuma yako, na lije jengine lisali nawe Swala iliyo bakia. Kisha litimize sehemu waliyo ikosa. Na lile la kwanza lisali baki ya Swala. Na hii huitwa "Laahiqah", yaani iliyo kutwa na nyengine inaitwa "Masbuuqah", yaani iliyo tanguliwa ,kwa kuwa inasaliwa mwanzo wa Swala ya Jamaa; na "Laahiqah" inasaliwa mwisho wa Swala ya Jamaa. Mpango huu ni kwa sababu isikosekane Swala, na kutahadhari na makafiri ambao wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu wapate kukuvamieni kwa ghafla, na wakumalizeni nanyi mmo katika Swala. Vita na washirikina ni waajibu, na havina ukomo. Lakini hapana dhambi juu yenu kusita kwa ajili ya udhuru kama mvua au maradhi, juu ya kuwa lazima muwe na hadhari ya kudumu. Na hii ni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa makafiri hapa duniani, na Akhera amewaandalia adhabu ya fedheha na udhalili. "Laahiq" ni anaye swali na Imam mwanzo wa Swala na akalazimika kusali iliyo baki peke yake, na "Masbuuq" anaye iwahi sehemu ya mwisho ya Swala ya Jamaa, kisha akatimiza sehemu aliyo ikosa peke yake.
Na mkisha Swala ya vita, inayo itwa Swala ya Khofu, msisahau kumkumbuka Mwenyezi Mungu daima. Mkumbukeni nanyi mmesimama, mnapigana, mmekaa, na mmelala. Kwani kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu kunatia nguvu nyoyo, na kuzituliza. Khofu ikiondoka pakawa na utulivu basi timizeni Swala kwa ukamilifu, kwani Swala imefaridhiwa juu ya Waumini isaliwe kwa nyakati zake.
Msilegee kuwafukuzia makafiri walio kwisha kukutangazieni vita na wanajaribu kukushambulieni kila pahala. Hakika vita havikosi maumivu. Ikiwa nyinyi Waumini mmepata majaraha na mengineyo, na wao makafiri pia wameyapata machungu. Khitilafu yenu ni kuwa wao hawapiganii Haki, wala hawataraji kitu kwa Mwenyezi Mungu; na nyinyi mnataka Haki na mnataraji radhi za Mwenyezi Mungu na neema za kudumu. Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu na vyao, naye ni Mwenye hikima, anamlipa kila mtu kwa alitendalo.
Tumekuteremshia hii Qur'ani kwa haki na kwa kweli. Imekusanya kila lilio la haki. Inabainisha haki mpaka Siku ya Kiyama, ili iwe ni taa yako ya kukupa mwangaza kuwahukumu watu. Basi hukumu baina yao, wala usiwepiganie walio makhaaini.