Na hakika Jihadi pamoja na kuchukua hadhari inayo takikana ina fadhila kubwa sana. Basi hawawi sawa wanao kaa majumbani mwao wasende kupigana Jihadi na wale Mujaahidiina, wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao. Kwani Mwenyezi Mungu amewanyanyua wale Mujaahidiina daraja, cheo cha juu kuwashinda wale wanao kaa nyuma; ila ikiwa wale wanao kaa nyuma wana udhuru unao wazuia kutoka kwenda vitani. Hapo inakuwa udhuru wao unawatoa lawamani, juu ya kuwa wanao pigana wana fadhila na cheo makhsusi. Mwenyezi Mungu amewaahidi makundi yote mawili mashukio mema, na matokeo mazuri.
Na cheo hichi walicho khusishwa nacho hao wanao pigana Jihadi ni cheo kikubwa, cha juu, hata imekuwa ni kama cheo cha kutafautisha sana baina yao na wengineo. Na kwa ajili ya cheo hichi watapata maghfira makubwa na rehema kunjufu.
Na hakika ni waajibu wa Muislamu kuhamia kwenye dola ya Kiislamu asiishi katika udhalili. Malaika watawauliza wakisha kufa: Mlikuwaje hata mkaridhia maisha ya unyonge na kudharauliwa? Na wao watajibu: Tulikuwa wanyonge katika nchi hiyo tukionewa. Malaika watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa kunjufu ina wasaa, mkaweza kuhama badala ya kuishi katika uonevu? Watu hao wanao kubali uonevu, na wao wanaweza kuondoka, makao yao yatakuwa ni Jahannamu. Na hayo ni mashukio maovu kabisa. Basi Muislamu haimfalii kuishi katika udhalili, bali aishi na utukufu wake na hishima yake.
Juu ya hivyo wanasameheka na adhabu hii wale wasio weza kusafiri miongoni mwa wanaume, na wanawake, na watoto, wasio na nguvu, na hawana hila, wala hawakupata njia ya kutoka.
Na hao wanatarajiwa kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu. Na ni shani yake Mwenyezi Mungu kusamehe na kughufiria.
Anaye hama kutafuta njia za kuiwania Haki na kuiunga mkono, atakuta duniani kwingi endako ambako maadui wa Haki wanahizika. Na atapata wasaa wa uhuru, na makao ya hishima,na thawabu, na ujira mkubwa. Aliye toka kwake kuhamia dola ya hishima, ambayo ndiyo dola ya Mwenyezi Mungu na Mtumewe, kisha yakamdiriki mauti kabla hajafika endako, basi ujira wake umethibiti. Mwenyezi Mungu amemkirimu kwa kujiwajibishia kumlipa ujira wake, na kumghufiria na kumrehemu. Ni shani yake kughufiria na kurehemu.
Swala ni faridha isiyo epukika. Haiachiki Swala kwa ajili ya safari, lakini hana dhambi anaye fupisha Swala safarini. Watokao kwenda safari wakikhofia kuwa makafiri watawaletea ya kuwaudhi, wanaweza kufupisha Swala. Swala za rakaa nne zisaliwe rakaa mbili. Kutahadhari na kuingiliwa na makafiri ni waajibu, kwani wao ni maadui, na uadui wao uwazi.