Na mwanamke akikhofia kuwa mumewe anapuuza mambo ya nyumbani au anayatupa, hayajali, wala hayashughulikii, basi hapana dhambi kwa wote hao wawili kutafuta njia za kusuluhiana kwa mapatano mema na kukurubiana. Na mwenye akili kati yao ni yule anaye anza kutaka masikizano. Na suluhu daima ina kheri, haina shari ndani yake. Linalo zuia masikizano ni kule kuwa kila mmoja kung'ang'ania haki yake kwa ukamilifu, na ugumu na uchoyo wa nafsi unapo wamiliki watu. Wala hapana njia ya kurejeza mapenzi ila mmojapo kati ya wawili kulegeza kamba. Na huyo ndiye mwema, mchamngu, mwenye kujihifadhi na dhulma. Na mwenye kutenda vitendo vyema na akamcha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu anayo khabari ya vitendo vyake, na atamlipa kwavyo.
Kuwafanyia uadilifu wake kwa mapenzi ya daima yasiyo chafuliwa na udanganyifu, na kutendeana usawa katika mapenzi ikawa nipe nikupe, ni jambo lisilo wezekana kuwa. Kadhaalika haiwezi kuwepo usawa katika kuwapenda wake, ikiwa kuna zaidi kuliko mke mmoja. Walakini mkijitahidi, basi msimfanyie ujeuri mmoja wapo, mkamili upande mmoja, na mkamwacha mwengine si mke si mt'alaka. Yapasa mjitengeneze, na muendeshe nyumba zenu kwa wema si kwa ufisadi. Na mcheni Mwenyezi Mungu apate kughufirieni na akurehemuni. Ni shani yake kughufiria na kurehemu.
Ikiwa suluhu haikumkinika na ikawa chuki (au karaha) imeshika nguvu zaidi, basi inalazimika kufarikiana. Na wakifarikiana Mwenyezi Mungu atawatosheleza kila mmoja wao kutokana na ukunjufu wa rehema yake na fadhila yake. Na riziki ziko katika mikono ya Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye Mwenye hikima, na hupanga mambo yote kwa mipango yake.
Kiini cha Dini ni kumnyenyekea Mwenye kuumba ulimwengu, Mwenye utukufu na ukarimu, na kuukubali ufalme wake usio na ukomo. Kwani ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi. Na kwa huu Ufalme usio na ukomo amesema: Tumewausia watu wa dini zilizo toka mbinguni, katika Watu wa Kitabu na nyinyi Waislamu, mumkhofu Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na msiwe mnakufuru katika ibada yake, maana Yeye ndiye Mwenye utawala mkubwa kushinda wote. Hapana kitu kilicho toka nje ya utawala wake. Yeye ni Mkwasi, yaani mwenye kujitosha wala hakuhitajiini nyinyi. Juu ya hivyo Yeye anakuhimidini kwa imani yenu, kwani kwa kuwa Yeye ni Mwenye kujitosheleza mwenyewe, juu ya hivyo anasifu na kushukuru vitendo vyema vya waja wake.
Kupanga kila kitu cha mbinguni na duniani ni kazi ya Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka. Yeye ndiye Mwenye madaraka, Mwenye kuendesha, Mwenye kupanga. Yatosha kuwa Yeye ndiye Mtawala aliye amrisha ulimwengu ukajipanga ulivyo jipanga, na akawaamrisha watu wamuabudu, na wamtegemezee Yeye mambo yao, na wamche Yeye.
Hakika nyinyi enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Mko chini ya ufalme wa Mwenyezi Mungu Mwenye uweza na Mwenye nguvu. Akipenda atakufisheni na alete wengine kabisa. Na Yeye Mwingi wa Utukufu ni Muweza wa hayo, na Muweza wa kila kitu.
Na watu, pindi wakitafuta neema za dunia zilizo halali kwa njia ya haki iliyo nyooka sawa, basi hakika Mwenyezi Mungu atawapa neema za duniani na Akhera; kwani Yeye ndiye aliye miliki neema zote mbili.