Vipi inakufalieni kuwa msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na hali wanyonge, wanaume na wanawake na watoto wao, wanayayatika kuomba msaada wa kuwanusuru, huku wakimwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu wakisema: Ewe Mola Mlezi wetu! Tutoe kwenye utawala wa hawa madhaalimu, na kwa nguvu zako na rehema yako tuwezeshe tuwe chini ya utawala wa Waumini; na tujaalie kutoka kwako mgombozi wa kutunusuru!
Walio isadiki Haki na wakaifuata, hupigana kwa ajili ya kulitukuza Neno la Mwenyezi Mungu, na uadilifu, na Haki. Na wale wanao pinga wakafanya inadi hupigana kwa ajili ya dhulma na uharibifu. Kwa hivyo hawa wamekuwa ni vipenzi vya Shetani. Basi enyi Waumini! Wapigeni vita hao, kwani wao ni wenzake Shetani na wasaidizi wake. Na jueni kuwa nyinyi mtawashinda tu kwa kuungwa mkono na Mwenyezi Mungu, kwani mpango wa Shetani, na ingawa mkubwa vipi ufisadi wake, ni dhaifu, hauna nguvu. Na Haki ndiyo yenye ushindi.
Ewe Muhammad! Hebu huwaangalii ukawastaajabia wale walio taka kupigana kabla ya kuja ruhusa, wakaambiwa: Bado haujafika wakati wa vita. Basi izuieni mikono yenu msipigane. Bali shughulikieni kushika Swala, na kutoa Zaka. Na Mwenyezi Mungu alipo waamrisha wapigane kikawa kikundi kimoja kati yao kikawa kinawaogopa watu kama kumkhofu Mwenyezi Mungu, au zaidi. Wakasema kwa kuona ni mageni hayo: Kwa nini ukatuamrisha kupigana? Wao walidhani kuwa kuamrishwa vita kunahimiza ajali yao, na kwa hivyo wakasema: Hebu lau ungeli tungojea muda kidogo tupate kustarehe na ulimwengu! Waambie: Songeni mbele mkapigane hata ikiwa mtakufa mashahidi, kwani starehe ya dunia, ingawa ni kubwa vipi, ni chache ukilinganisha na starehe ya Akhera. Na Akhera ni bora na kubwa zaidi kwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, na huko mtakuja lipwa kwa vitendo vyenu vya duniani, wala hampunguziwi hata chembe katika ujira wenu.
Hakika hayo mauti mnayo yakimbia yatakukuteni popote pale mlipo, na hata mkikaa ndani ya ngome zilizo jengwa madhubuti imara. Na hao wenye imani legevu na dhaifu husema pindi wapatapo ushindi na ngawira: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na pindi wapatapo lawama au kushindwa wao hukwambia wewe: Ewe Muhammad! Haya yanatokana na wewe. Haya si lolote ila kukufanya kuwa wewe ni mkorofi, na kukutupia lawama wewe badala ya nafsi zao. Basi waambie: Kila linalo kupateni, mnalo lipenda na mnalo lichukia, linatokana na kudra ya Mwenyezi Mungu, na linatokana na majaribio yake na mitihani yake. Wana nini watu hawa madhaifu hata hawajakaribia kujua usawa wa maneno wanayo ambiwa?
Ewe Nabii! Kufanikiwa, na neema, na afya, na salama unayo ipata inatokana na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako. Yeye anafanya haya kukufadhili kukufanyia hisani. Na inapo kusibu shida, na mashaka, na udhiya, na ya karaha, basi yanatokana na nafsi yako mwenyewe kwa sababu ya upungufu fulani au makosa uliyo yatenda. Haya anaambiwa Mtume s.a.w. ni kama mfano wa wanaadamu wote ijapo kuwa halikutokea kwake la uovu. Kwani Mtume anaambiwa: Tumekutuma kuwa Mtume kutoka kwetu kwa watu wote. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kufikisha kwako huo ujumbe na juu ya kuitikia kwao hao watu. Na Yeye ni Mjuzi wa kutosha.