Huu ndio mwisho wa wafuasi wa Shetani. Ama mwisho wa wafuasi wa Mwenyezi Mungu ni mzuri. Wao ndio walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda mema, wala hawazugwi na mawazo ya uwongo. Hakika Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu Mtukufu atawatia katika mabustani yapitayo mito kati yake, chini ya vivuli. Na hayo ni makubwa mno kuliko bustani hizi za duniani. Na hayo ni yakini, kwani ahadi hizo ni ahadi za Mwenyezi Mungu, na ahadi zake haziwi ila ni hakika isiyo geuka, wala haina udanganyifu. Yeye ni mmiliki wa kila kitu. Wala haiwezi kufikirika kuwa yupo yeyote yule aliye mkweli kwa neno lake na ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu.
Malipo siyo ayatamaniyo mtu na kuyaota bila ya vitendo vyema vizaavyo matunda. Malipo siyo myatamaniyo nyinyi, Waislamu. Wala siyo wayatamaniayo na kuyaota Ahlu-l-Kitabi, Watu wa Biblia, Mayahudi na Wakristo. Bali malipo na kuepukana na adhabu ni kwa Imani na Vitendo Vyema. Atendaye maovu atalipwa kwa vitendo vyake. Wala hampati mlinzi wala wa kumnusuru ila Mwenyezi Mungu.
Watendao mema, kwa kadiri ya uwezo wao nao wanamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wataingia kwenye Pepo ya neema, wala hawatapunguziwa hata chembe. Na hapana khitilafu baina ya malipo ya mwanamume na ya mwanamke, kwani mwanamke naye ana waajibu wake, malipo ya vitendo vyema, na adhabu kwa vitendo vibaya.
Msingi wa vitendo vyema ni itikadi iliyo sawa. Na bora ya dini ni kumtakasikia niya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ukawa uso wako, na akili yako, na nafsi yako, yote haitaki kitu isipo kuwa kumridhi Mwenyezi Mungu Subhanahu. Kwa hivyo basi ndio fahamu zako zitanyooka sawa kuufahamu ujumbe wa Mitume, na ndio utaweza kushika daima vitendo vilivyo bora, na ukamfuata Baba wa Manabii, Ibrahim a.s. Kwani dini yake Ibrahim ndiyo Dini ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo Dini inayo elekeza kutaka Haki daima. Na kwa Ibrahim ndiyo umekutana umoja wa Dini, kwa Waislamu, na Mayahudi na Wakristo. Basi ifuateni njia yake. Mwenyezi Mungu hakika amemkirimu Ibrahim, akamwita "Rafiki Mwendani".
Hakika wa kumtakasia niya ni Mwenyezi Mungu, na ndio kwake Yeye inapasa uusilimishe uso wako, yaani umuelekee na umnyenyekee. Huko ndiko kumsafia niya Mwenyezi Mungu aliye umba ulimwengu wote, na ndiye mwenye kuumiliki. Vitu vyote viliomo mbinguni na duniani - nyota, sayari, jua, mwezi, milima, mabonde, majangwa, mashamba n.k. ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kubainikiwa na kila kitu, Mwenye kujua kwa ujuzi mkamilifu wa kuvizunguka vitu vyote avitendavyo mwanaadamu. Na Yeye atamlipa kheri akitenda kheri, na shari akitenda shari.
Watu walimtaka Mtume s.a.w. awambie nini hukumu ya sharia juu ya wanawake. Na wanawake walikuwa, na wangali bado kuwa, ni watu wanyonge. Basi Mwenyezi Mungu amembainishia Nabii wake ili naye abainishe hali ya wanawake, na hali ya wanyonge wengine katika ukoo miongoni mwa watoto na mayatima. Na akataja kuwa mayatima wanawake ambao wanaolewa wala hawachukui mahari yao, na watoto, na mayatima, wote hao watendewe kwa uadilifu na huruma na kuraiwa. Na kwamba kila kheri itendwayo basi hakika Mwenyezi Mungu anaijua, na Yeye ndiye atakaye ilipa.