Na makafiri wa Makka wamejaribu, na walikaribia kukuudhi mpaka wakutoe kwenye ardhi ya Makka kwa uadui wao na chuki zao. Na lau yangeli kuwa hayo, basi wao nao wasingeli baki humo ila muda mchache tu, kisha washindwe katika hayo mambo yao, na hukumu iwe ya Mwenyezi Mungu.
Na huo ndio mwendo wetu kwa Mitume wa kabla yako - huwahiliki wale wanao wafukuza Manabii wao. Na wala hapana mabadiliko katika mwendo wetu.
Shika Swala zilizo faridhiwa, tangu kupinduka jua kati ya mbingu kuelekea upande wa machwea jua, mpaka kiza cha usiku. Na hizi ndizo Swala za Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha. Na pia shika Swala ya Alfajiri ambayo wanaishuhudia Malaika.
Na katika wakati wa usiku amka, kwa kusali Swala ya Tahajjud. Hiyo ni ibada ya zaidi juu ya zile Swala Tano. Hii imekukhusu wewe tu, kwa kutaraji kuwa Mola wako Mlezi atakuweka Siku ya Kiyama makamo watakao kusifia viumbe.
Na sema: Ewe Mola Mlezi! Niingize maingizo ya kuridhisha matukufu katika kila unapo niingiza katika jambo au pahala. Na unitoe kwa kutoka kunako ridhisha kutukufu. Na kwa fadhila yako nijaalie nguvu za kunisaidia niwashinde maadui zangu.
Na sema ukiwaonya watu wako washirikina: Haki ya Tawhid, Imani ya Mungu Mmoja, na Dini ya Kweli na Uadilifu, imekwisha fika. Na uwongo, na ushirikina, na dini ya ufisadi na dhulma, yote hayo yameondoka. Kwani uwongo daima hauna dawamu.
Na vipi Haki isiwe na nguvu na hali Sisi tunateremsha katika Qur'ani dawa ya kuponyesha maradhi ya shaka katika vifua vya watu, na sababu za kuwapatia rehema wanao iamini! Na madhaalimu hawana linao wazidia ila khasara tu kwa kuikataa kwao.
Na hakika katika maumbile ya mwanaadamu ni kujidanganya na kukata tamaa. Tukimneemesha kwa kumpa uzima na ukunjufu wa mali, hupuuza kutukumbuka na kutuomba, na hujitenga nasi kwa kiburi na majivuno! Na akiguswa na shari, kama ugonjwa na ufakiri, huwa mwingi wa kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Ewe Nabii! Waambie makafiri wa Kikureshi kwa kuepuka kuchochea ugomvi na makindano: Kila mmoja wetu na mmoja wenu anatenda na anakwenda kwa kufuata njia yake. Na Mola wenu Mlezi ni Mjuzi mno, wala hana ajuaye kuliko Yeye kumjua nani aliye shika njia sawa na kufuata Haki. Na huyo humlipa ujira wake kaamili. Na kumjua aliye potea njia, na huyo humpa adhabu kama anayo stahiki.
Ewe Muhammad! Watu wako wanakuuliza kwa kutomezwa na Mayahudi: Nini hakika ya Roho? Waambie: Roho ni katika ilimu yake Mwenyewe Mola wangu Mlezi aliyo jikhusisha nayo Yeye. Na nyinyi hamkupewa ilimu ila chache tu ukilinganisha na ilimu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na lau tungeli taka kuifuta kabisa kifuani mwako hiyo Qur'ani tuliyo kufunulia tungeli fanya hivyo, na kisha usingeli mpata yeyote wa kukunusuru katika watu wako.