Watu wako wamekutaka uwaletee Ishara na miujiza. Nao hawakukinaika kwa yaliyo wajia ambayo huwakinaisha wenye akili. Na mwendo wetu umekwisha wapitia hao wanao taka miujiza, na wanapo kubaliwa wasiamini, nao ni kuwang'olea mbali kwa adhabu kama tulivyo wafanyia wa kale. Miongoni mwa hao ni watu wa Thamud. Walitaka miujiza, akawa ngamia mke ni muujiza wazi kwao wa kuondoa shaka zote. Wakamkanusha, yakatokea kwao yaliyo tokea! Na imekuwa hikima ya Mwenyezi Mungu kuwa asiwakubalie hayo waliyo yataka, kwa kuchelea wasiikatae miujiza, kwa kutarajia watakuja amini miongoni mwao, au watakuja zaa watakao amini. Na miujiza hakika Sisi huwapelekea watu kwa kuwatia khofu na kitisho.
Ewe Nabii! Kumbuka tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amewazunguka hao watu. Wao wamo wamedhibitiwa na kudra yake. Basi wewe wafikishie Ujumbe wala usimwogope yeyote katika wao. Mwenyezi Mungu atakulinda nao. Na mambo ya ajabu uliyo yaona katika Usiku wa Israi (Safari ya Usiku), hatukuyafanya Sisi ila yawe ni mtihani na majaribio kwa wanaadamu. Kwa hayo ipate kuzidi Imani ya Muumini, na ukafiri wa kafiri. Na wala hatukuufanya ule mti ulio subiwa katika Qur'ani, nao ni Mti wa Zaquum, unao mea huko Motoni, isipo kuwa ni kuwafanyia wao pia mtihani pale walipo sema: Moto unaunguza mti, basi vipi mti umee katika moto? Pia ni kuzidi kuwahadharisha kwa hayo. Lakini kuwahadharisha kwetu hakuwazidishii isipo kuwa kupindukia kiwango kikubwa kabisa.
Na Mwenyezi Mungu anakumbusha asli ya kuumba na uadui baina ya mwanaadamu na Iblisi, pale alipo waambia Malaika: Msujudieni Adam kwa kumuamkia na kumhishimu kwa kumuinamia. Hapo hapo wakasujudu. Isipo kuwa Iblisi akakataa, na akasema kwa chuki: Vipi nimsujudie uliye muumba kwa udongo, na hali mimi umeniumba kwa moto. Mimi ni bora kuliko yeye.
Iblisi akasema: Ewe Mola wangu Mlezi hebu ni ambie khabari za huyu uliye mtukuza juu yangu, ukaniamrisha ni msujudie kwanini kamtukuza kuliko mimi, na mimi ni bora kuliko yeye, Naapa kwa utukufu wako. Ukinibakisha ni hai mpaka siku ya Kiyama, basi nitawahiliki dhuria zao watao wazaa kwa kuwaghuri isipokwa wachache tu, kati yao utakao walinda na Kuwahifadhi.
Mola akamwambia kwa kumtisha na kumlegezea kamba: Endelea na shani yako uliyo jichagulia kuifuata. Atakaye kut'ii wewe katika wana wa Adam, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yako na yao, malipo ya kutosha yaliyo kamilika.
Na wazuge na wavute kwa kuwaita wamuasi Mwenyezi Mungu hao unao waweza miongoni mwao. Na fanya kila juhudi yako ya namna zote za udanganyifu. Na shirikiana nao katika kuchuma mali ya haramu, na kuyatumia kwa haramu, na kuwakufurisha watoto na kuwaghuri wafanye fisadi. Na wape ahadi za uwongo, kama kuwa miungu yao itawaombea, na kuwa watapata utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya nasaba zao. Na Shetani hawaahidi wafwasi wake ila kwa udanganyifu na uficho.
Ama waja wangu walio nisafia niya Mimi wewe huna uwezo wa kuwapotoa, kwa kuwa wao wanamtegemea Mola wao Mlezi. Na Yeye anatosha kabisa kuwa ni wa kuwanusuru wakimtaka msaada wa kusalimika nawe.
Mola wenu Mlezi ni Yeye peke yake ndiye anaye ziendesha marikebu baharini ambazo kwazo nyinyi mnatafutia manufaa kwa biashara na mengineyo. Yeye daima ni Mwenye rehema kwenu.