Lakini tumeiacha Qur'ani ibaki vile vile kifuani mwako kwa rehema kutoka kwa Mola wako Mlezi, kwani fadhila zake kwako wewe ni kubwa mno katika muujiza huu.
Waambie, kwa kushindana nao, kama wanaweza walete mfano wake. Nao hawawezi! Hata wakikusanyika watu na majini wakasaidiana kuleta mfano wa hii Qur'ani kwa mpango wake na maana yake, hawawezi; na wanga saidiana wao kwa wao.
Na katika Qur'ani hii tumewaeleza watu kwa namna mbali mbali kila maana kama ni mifano katika maajabu yake. Lakini watu wengi walikataa ila kupinga na kuchukia.
Ilipo dhihiri kushindwa kwao na Qur'ani, na wakabanwa kwa hoja, wakataka waletewe ishara nyingine na miujiza mingine. Hicho ni kitendo cha mwenye kushindwa hoja, aliye emewa na kutahayari. Ndio wakasema: Hatutokuamini mpaka ututimbulie katika ardhi ya Makka chemchem ambayo maji yake hayakatiki.
Au uwe nacho kitalu Makka cha mitende na mizabibu chenye kupita mito kati yake! (Kwa kujua kuwa ardhi ya Makka ni kavu haioti kitu.)
Au mbingu ituangukie vichwani mwetu kwa mapande kama ulivyo dai kuwa Mwenyezi Mungu anatuahidi hayo. Au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika tukabiliane nao macho kwa macho!
Au uwe na nyumba iliyo pambwa kwa dhahabu, au upae mbinguni. Na hata hivyo hatukusadiki mpaka ukituletea kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha ukweli wako tukisome! Waambie: Mola wangu Mlezi ametakasika kabisa na kuhukumiwa na yeyote, au yeyote kushirikiana naye katika kudra yake! Mimi si chochote ila ni mwanaadamu kama Mitume wote wengineo. Na wala wao hawakuwaletea watu wao muujiza ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Na nini kilicho wazuilia washirikina wa Makka kuifuata Haki ulipo wajia wahyi (ufunuo) pamoja na miujiza isipo kuwa madai yao kwa ujinga wao ya kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hatumi Mitume wanaadamu, ila huwa ni Malaika!
Sema kwa kuwarudi: Lau kuwa duniani badala ya wanaadamu wapo Malaika wanatembea kama wanaadamu na wamekaa humo, basi tungeli wateremshia kutoka mbinguni Malaika kuwa ni Mitume wao katika jinsi yao. Lakini Malaika si kama binaadamu; na wangeli kuja basi wange kuja kwa sura za watu.
Sema: Kama mnaukataa Utume wangu, basi Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutuhukumu baina yangu na nyinyi, akathibitisha ukweli wa Ujumbe wangu kwenu. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kujua hali zenu, na Mwenye kuviona vitendo vyenu. Naye ni Mwenye kukulipeni kwa hivyo.