Waambie: Yule ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa kwa kuwa yu tayari kufuata uwongofu, basi huyo ni mwongofu. Na anaye mpotoa kwa kufisidika khulka yake, hutopata wa kuwanusuru asiye kuwa Yeye wa kuwaongoa duniani. Na Akhera tutawakusanya wakikokotwa juu ya nyuso zao, hawaoni, wala hawasemi, wala hawasikii. Na mahali pao wanapo pelekwa kukaa ni Jahannamu. Kula moto ukipungua ukali wake Mwenyezi Mungu anazidi kuuchochea uwake kwa nguvu zaidi.
Adhabu hiyo ndiyo malipo yao kwa sababu ya kuzikataa dalili tulizo waletea za kuthibitisha Haki, na kwa ile kauli yao kusema: Hivyo sisi tutafufuliwa kwa umbo jipya baada ya kwisha kuwa mifupa na vumbi?
Jee wameghafilika na hawakujua kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, juu ya ukubwa wao, ni Mwenye kuweza kuumba watu na majini kama wao? Na Mwenye kuweza hayo, vipi awe hawezi kuwarejesha wao upya, na hilo ni jepesi zaidi kwake! Na Yeye Subhanahu ameweka muda maalumu wa kuwarejesha tena baada ya kwisha kufa, na huo hauna shaka kuwa. Na muda huo ndio Siku ya Kiyama. Na juu ya hivyo walio zidhulumu nafsi zao kwa ukafiri wanakataa baada ya kuletewa hoja hizi. Na hayo si kwa lolote ila kwa ukafiri tu.
Waambie hawa washirikina: Lau kuwa mnazimiliki riziki za Mola wangu Mlezi, mngeli zifanyia ubakhili kwa kuogopa ufakiri. Kwani ni tabia ya watu kuwa na pupa na ubakhili. Na Mwenyezi Mungu, Mkwasi na Karimu, humpa anacho taka amtakaye, na huteremsha miujiza aitakayo Yeye, sio waitakayo watu. Na Yeye katika yote hayo ni Mwenye hikima na Mjuzi.
Na lau hawa watu wangeli letewa hizo ishara wazitakazo, wange zigeuzia uso, wala wasinge ziamini! Na Sisi tulimpa Musa Ishara tisa wazi. Na juu ya hivyo wakakufuru. Na Firauni akasema: Hakika mimi nakuona wewe, Musa, ni mtu uliye rogwa! Hizo ishara tisa ni: 1. Fimbo, 2. Mkono Mweupe, 3. Tufani, 4. Nzige na vyura na chawa na damu, 5. Ukame na upungufu wa mazao, 6. Kupasuka bahari, 7. Kutimbuka maji baharini, 8. Kuning'inia mlima kama kivuli, 9. Kusemezwa na Mola wake Mlezi.
Musa akasema: Ewe Firauni! Unajua vyema kuwa aliye ziteremsha Ishara hizi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Kwani ni Yeye ndiye Mwenye kuweza hayo. Nazo Ishara hizo zi wazi, zinakuonyesha ukweli wangu. Lakini wewe unafanya kiburi na inadi tu. Na hakika mimi nakuona wewe, Firauni, kuwa ni mwenye kuangamia ikiwa hutoacha inadi yako.
Firauni akashikilia uasi wake, akataka kumtoa Musa na Wana wa Israili katika nchi ya Misri. Tukamzamisha yeye na askari wake wote.
Tukamvua Musa na kaumu yake, na baada ya kumzamisha Firauni tukasema kuwaambia Wana wa Israili: Kaeni katika nchi takatifu ilioko Sham. Ukija wakati wa uhai wa pili tutakutoeni makaburini kwenu kwa mchanganyiko. Kisha tutakuhukumuni kwa uadilifu.