Na hayo ni katika aliyo kufunulia Mola wako Mlezi, katika kuijua haki kwa dhati yake, na kheri ipate kutendwa. Wala usimfanyie Mwenyezi Mungu kuwa na mungu mwengine, usije kutupwa katika Jahannamu ukijilaumu na ukilaumiwa, umeangamia na umefurushwa mbali na rehema za Mola wako Mlezi.
Subhanahu anayachukia wayasemayo makafiri kwamba Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu. Anasema: Mola wenu Mlezi amekufadhilisheni kuliko Mwenyewe kwa kukupeni nyinyi watoto wanaume wenye nguvu, na Yeye akawafanya Malaika ni banati zake kwa mnavyo dai? Kwa maneno yenu haya mnazua matusi makubwa.
Sisi tumebainisha katika Qur'ani hii kwa uwazi mzuri, tukipiga mifano na kutoa mawaidha na hukumu, ili wapate kwaidhika hawa washirikina. Lakini nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kubainisha huku hakukuwazidishia ila kuzidi kuwakimbiza na Haki.
Ewe Nabii! Ili kudhihirisha upotovu wa madai yao wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu, sema: Lau kuwa wapo miungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu kama wasemavyo, hao miungu wangeli tafuta njia kumfikilia huyo Mwenye Ufalme wa mwisho ili wapate kushindana naye.
Mwenyezi Mungu ametakasika kabisa kama anavyo stahiki, na ametukuka aliye mkuu shani yake na yote wanayo dai kuwa wapo pamoja na Yeye miungu wengine.
Hakika mbingu saba na ardhi, na viumbe vyote viliomo humo, vinamtakasa na kumtukuza, na vinaonyesha uzuri wa kuumba kwake, na kutakasika kwake Subhanahu na kila upungufu, na kukamilika ufalme wake, na kwamba Yeye hana mshirika na yeyote katika viumbe wa Ufalme wake uliyo enea. Vyote hivyo vinamtakasa na kumsifu. Lakini makafiri hawafahamu hoja hizi kwa kutawaliwa nyoyo zao na mghafala. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwao, na Mwenye kuwasamehe wanao tubu. Kwa hivyo hawafanyii haraka kuwapa adhabu.
Ewe Nabii! Unapo soma Qur'ani inayo taja dalili za Haki, Sisi huweka pazia, lenye kukuficha baina yako na wale wasio amini kufufuliwa na malipo, pale wanapo taka kukushambulia. Kwa hivyo hawakuoni.
Na kwa mujibu wa hikima yetu ya kupotoa na kuongoa huweka vifuniko juu ya nyoyo zao, wasipate kuifahamu Qur'ani ilivyo. Na katika masikio yao hutia uziwi basi hawasikii lenye manufaa kwao. Hayo ni kwa sababu ya kupindukia katika inda yao na majivuno yao. Na pale unapo mtaja Mola wako Mlezi katika Qur'ani peke yake bila ya kuwataja miungu yao, wao basi hurejea nyuma wakaacha kukusikiliza.
Sisi tunajua vyema vile wanavyo isikiliza Qur'ani nao ilhali wanaikejeli na kuifanyia maskhara na huku wanakusikiliza. Nao wanayaficha yaliyo semwa. Na hiyo ndiyo kauli ya wenye kudhulumu katika siri zao, wakisema: Ikiwa mtamfuata huyu basi hamumfuati ila mtu aliye geuzwa akili yake.
Hebu angalia vipi walivyo kushabihisha; wamekushabihisha na mtu aliye rogwa, na wakakuita kohani, mtunga mashairi, wakaipotea njia ya hoja. Kwa hivyo wasiweze kupata njia ya kuzua tusi linalo kubalika, au kwa hivyo wakaukosa uwongofu, na wasiipate njia ya kuufikilia.
Wanao kataa kuwa watafufuliwa wanasema: Hivyo tutafuliwa baada ya kwisha kuwa mafupa yaliyo bunguliwa, na mapande mbali mbali, tukawa hai na umbo jipya? Haya hayaingii akilini.