Na wakumbushe pia hao Mayahudi pale kikundi cha watu wema katika wenzao walio tangulia, ambao hawakutenda mabaya waliyo yatenda wengineo, walipo waambia wanao wapa mawaidha wale waovu: Kwa sababu gani mnawapa nasaha watu ambao Mwenyezi Mungu atawahiliki, au atawaadhibu adhabu kali Akhera, kwa sababu ya madhambi wanayo yatenda? Wakasema: Tunawapa mawaidha ili tupate udhuru kwa Mola wako Mlezi, tusiwe tumefanya taksiri, na kutaraji huenda wakamchamngu.
Walipo yaacha mawaidha waliyo pewa, tukawaokoa na adhabu wale ambao walikuwa wakikataza vitendo viovu, na tukwashika walio dhulumu na wakavuka mipaka na wakakhalifu kwa kuwapa adhabu kali, nayo ni udhalili na shakawa, kwa sababu ya kuendelea kwao kutokana na ut'iifu wa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wao.
Walipo zidi kuwa wagumu, na wakaendelea kutobali waliyo katazwa, wala adhabu kali isiwaachishe uovu, tukawafanya kama manyani kwa kuzigeuza nyoyo zao, na kuwaondolea uwezo wa kuifahamu Haki, wakawa mbali na kila kheri.
Na wakumbushe pia hao Mayahudi pale alipo wajuvya Mola Mlezi wako wenzao walio watangulia kwa ndimi za Manabii wao: Mwenyezi Mungu atawasalitisha Mayahudi mpaka Siku ya Kiyama adhabu mbaya kabisa kwa sababu ya dhulma yao na upotovu wao. Kwani Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuwaadhibu watu makafiri, kwani adhabu yake itakuja tu bila ya shaka yoyote. Na kila kijacho kipo karibu, (chambilecho Waarabu). Na Yeye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu kwa anaye rejea kwake akatubu.
Na Sisi tumewagawa makundi makundi duniani. Wamo kati yao walio wema. Na hao ndio walio amini wakenda mwendo ulio sawa. Na wapo miongoni mwao watu wasio sifika kwa wema. Na wote tumewafanyia mitihani kwa kuwapa neema na kuwapa nakama, ili watubu, waache waliyo katazwa.
Baada ya hao tulio kwisha wataja na tukawagawa sehemu mbili, walifuatia waovu wakairithi Taurati kutokana na walio watangulia. Lakini hao hawakufanya yalio amrishwa humo. Kwani wao walishika starehe ya dunia badala ya Neno la Haki. Wakijiambia nafsi zao: Mwenyezi Mungu atatusamehe kwa tunayo yatenda! Wakitaraji maghfira, na ilhali kuwa yakiwajia kama yale waliyo yashika watayashika vile vile. Basi wao wamekuwa wameshikilia kuendelea na madhambi pamoja na kutaka kwao msamaha. Tena basi Mwenyezi Mungu anawatahayarisha kwa vile kutaka maghfira na huku wanaendelea na yao, akasema: Sisi tulichukua kwao ahadi katika Taurati - nao wameyasoma yaliomo humo - kuwa waseme kweli; nao wakasema uwongo! Na hakika neema za nyumba ya Akhera za wanao jikinga na maasi ni bora kuliko starehe za duniani! Basi je, mtaendelea na uasi wenu, wala hayaingii akilini mwenu kuwa neema hizo ni bora kwenu? Na mnakhiari badala yake hizo starehe za dunia?
Na wanao ikamata baraabara Taurati, na wakashika Swala zilizo faridhiwa kwao, hakika Sisi hatutaupoteza ujira wao kwa sababu ya kutengeneza kwao na kutenda kwao mema.