Na haikuwa jawabu ya watu wake kwa kukatazwa hichi kitendo kiovu kisicho kuwa na mfano, ila ni kusema: Watoeni Lut' na jamaa zake na wafuasi wake katika mji wenu! Nayo ni kwa kuwa wao wanajitahirisha na wanajitenga na hichi kitendo ambacho akili na maumbile yanakiona ni kibaya, na wao hao watu wanakioni kizuri!
Amri ya kuadhibiwa ilikwisha thibiti. Basi Sisi tukamwokoa Lut' na watu wake, isipo kuwa mkewe, kwani yeye alikuwa katika hao walio potea.
Basi tuliwateremshia mvua ya mawe ya kuteketeza, na ardhi ikatandazwa kwa mitetemeko ya chini yao! Basi ewe Nabii! Angalia vipi ulikuwa mwisho wa wakosefu.
Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao, Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Hoja zilizo wazi za kuthibitisha Haki inayo toka kwa Mola Mlezi wenu juu ya Utume wangu kwenu zimekwisha kujieni. Na umekujieni Ujumbe wa Mola wenu Mlezi kwamba mtengeneze kwa uadilifu maingiliano yenu nyinyi kwa nyinyi. Basi timizeni vipimo na mizani mnapo uziana, wala msipunguze haki za watu, wala msiiharibu nchi nzuri, kwa kufisidi mapando na kadhaalika, na kuwatenga jamaa na kuondoa mapenzi. Kwani hayo ni bora kwenu mkiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mnaamini Haki iliyo wazi.
Wala msikae katika kupinga kila njia za Haki na uwongofu na a'mali njema, mkiwatishia wapitao, na kwa hivyo mkawazuia watafutao kheri wasiifikie. Nao hao ndio watu wa Imani wanao muamini Mwenyezi Mungu, nanyi mnaitaka njia iliyo potoka! Na kumbukeni mlivyo kuwa ni watu wachache, Mwenyezi Mungu akakufanyeni mkawa wengi kwa kwenda sawa kutaka uzazi na mali. Na zingatieni nini ulikuwa mwisho wa waharibifu walio kuwa kabla yenu.
Ikiwa kipo kikundi kati yenu kilicho amini Haki niliyo kuja nayo, na kikundi kingine hakikuamini, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete hukumu yake baina ya pande mbili hizo. Naye ndiye Mbora wa mahakimu.