Na lau kuwa watu wa hiyo miji wangeliamini walio kuja nayo Mitume, na wakatenda walio wausia, na wakajitenga na aliyo yaharimisha Mwenyezi Mungu, tungeli wapa baraka nyingi zitokazo mbinguni na kwenye ardhi, kama mvua, na mimea, na matunda, na wanyama, na riziki, na amani na kusalimika na misiba. Lakini wao wakapinga na wakawakadhibisha Mitume. Basi tukawapatiliza kwa adhabu nao wamelala, kwa sababu ya ukafiri na maasi waliyo yazua. Basi huko kushikwa waliko shikwa kwa adhabu ni matokeo ya lazima kuwa kwa ajili ya maovu waliyo yachuma, na yawe kuwa ni somo kwa walio kama wao ikiwa wanayatia akilini!
Je, watu wa hii miji walio letewa wito wa Manabii wao na wasiwaamini, wamejiaminisha kuwa adhabu yetu haitawafika nao wamezama katika usingizi wao?
Je, watu hawa wameghafilika na wamejiaminisha kuwa adhabu haitawajia mchana kweupe na jua linawaka, nao wameshughulikia mambo yasiyo na faida nao?
Je, hawaujui mwendo wa Mwenyezi Mungu anavyo kwenda nao wanao kanusha, hata wakajitumainisha kuwa haitowafikia adhabu usiku au mchana? Naye, huipeleka kwa mpango wake wasio uona watu. Hakika hawawi wajinga wa mpango na mwendo wa Mwenyezi Mungu katika kuadhibu ila wale wanao kanusha, wenye kuzikhasiri nafsi zao kwa kutozinduka katika mambo yaliyo khusu kufanikiwa kwao.
Je, hawaujui mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa kaumu zilizo kwisha pita kabla yao, na kuwa shani yetu kwao ni kama ilivyo kuwa kwa walio watangulia? Na kwamba wao lazima wafuate tuyatakayo. Tukitaka kuwaadhibu kwa sababu ya madhambi yao tutawapatiliza kama tulivyo wapatiliza walio kama wao. Nasi tunatia muhuri nyoyo zao kwa kuwa zimeharibika bila ya kiasi, mpaka ikafika ukomo kuwa hazipokei tena uwongofu. Kwa muhuri huo imekuwa hawasikii hikima wala nasiha, kwa msikio wa kufahamu na kuwaidhika.
Hiyo ni miji iliyo dumu karne nyingi, na imepitiwa na muda mrefu katika taarikhi yao. Tunakusimulia hivi sasa baadhi ya khabari zao zenye somo la kuzingatiwa. Na watu wa miji hiyo walifikiwa na Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi zenye kuonyesha ukweli wa wito wao. Lakini haikuwa shani yao kuamini baada ya kuja hizo Ishara zilizo wazi, kwa sababu ya mtindo wao wa kuwakanusha wasemao kweli. Basi wakawakadhibisha Mitume wao, wala hawakuongoka! Basi ni hivyo Mwenyezi Mungu huweka kizuizi juu ya nyoyo na akili za makafiri, ikafichika kwao Njia ya Haki, na wakajitenga nayo.
Wala hatukuwakuta wengi wa watu hao kuwa ni wenye kutimiza ahadi kwa Imani tulio wausia kwa ndimi za Mitume, na yanayo tambuliwa na akili na nadhari nzuri. Na mwendo ulio thibiti kwao ni vile kuselelea katika upotofu na kwenda kinyume na kila ahadi.
Tena baada ya Mitume hao tulimtuma Musa a.s. Naye akaja na dalili zenye kuonyesha ukweli wa anayo yafikisha kutokana nasi kumpelekea Firauni na kaumu yake. Musa akaufikisha wito wa Mola wake Mlezi, na akawaonyesha Ishara ya Mwenyezi Mungu. Nao wakadhulumu nafsi zao na watu wao kwa kuzikataa kwa kiburi na upinzani tu! Basi wakastahiki adhabu kali kutokana na Mwenyezi Mungu, na hivyo ukawa mwisho wa mambo yao! Basi ewe Nabii! Angalia vyema mwisho wa mafisadi katika ardhi.
Musa akasema: Ewe Firauni! Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, Mwenye mamlaka juu ya mambo yao yote, ili nikufikishieni wito wake, na nikuiteni muifuate Sharia yake.