Na tumewaumbia wengi katika majini na watu marejeo yao ni Motoni Siku ya Kiyama. Kwani hao wana nyoyo zisio funguka ikaingia Haki ndani yake. Wana macho yasiyo angalia dalili za kudra. Wana masikio yasiyo sikia Aya na mawaidha kwa sikio la kuzingatia na kuwaidhika! Hao ni kama wanyama kwa kutonafiika kwa neema ya akili za kuzingatia walizo neemeshwa na Mwenyezi Mungu. Bali hao ni wapotovu zaidi kuliko wanyama, kwani wanyama hutaka cha kuwafaa na hukimbia cha kuwadhuru. Lakini hawa watu hata hawatambui hayo. Hao ndio walio fikia ukomo wa kughafilika.
Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye Majina yenye kuonyesha sifa za ukamilifu. Basi mtumilieni hayo mnapo muomba, au mnapo mwita au kumtaja. Na waepukeni hao wanao mili katika hayo yasiyo elekeana na dhati ya utukufu wake. Hao watakuja lipwa malipo ya vitendo vyao.
Na katika tulio wajaalia waingie Peponi wapo wanao waita wengineo kwenye Haki kwa kuipenda Haki, na kwa Haki tu wanafanya uadilifu katika hukumu zao.
Na wale walio zikanusha Ishara (Aya) zetu zilio teremshwa tutawapururia pole pole, na tutawawacha mpaka wafike ukomo watapo fika. Na hayo ni kwa kuwapururia neema juu yao, juu ya kushughulika kwao katika maasi, mpaka maangamizo yawazukie nao wameghafilika wakitaladhadhi na starehe zao.
Wao wameanza kwa kukadhibisha, wala hawakuzingatia yale anayo waitia kwayo Mtume, na hoja anazo zitoa. Bali wakamsingizia kuwa ni mwendaazimu, na hali hana wazimu chochote. Yeye huyu ni mwenye kuwaonya wasifikiwe na adhabu ya ushirikina wao. Na onyo lake liwazi, la dhaahiri.
Wamemwambia Muhammad mwongo kwa Tawhidi anayo waitia, wala hawakutazama kwa kuzingatia na kutafuta dalili za ufalme mtukufu wa Mwenyezi Mungu ulioko katika mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, zinazo onyesha ukamilifu wa uwezo wa huyu Mwenye kuunda, na zinazo onyesha Umoja wake wa pekee. Wala hawakufikiri kuwa ajali yao imekwisha karibia, au huenda ikawa imekaribia, wapate kufanya haraka kutupia nadhari na kuitafuta Haki kabla ya kuzuka ajali. Ikiwa basi watu hawa hawaamini maneno ya Qur'ani watakuja amini maneno gani baada yake
Aliye andikiwa na Mwenyezi Mungu kupotea kwa uwovu wa uchaguzi wake mwenyewe, basi hapana mtu wa kumhidi. Na Yeye Subhana, Aliye takasika, anawaacha watu kama hao wakihangaika wala hawaitambui njia.
Ewe Muhammad! Mayahudi wanakuuliza khabari ya Saa itakayo malizikia dunia. Itakuwa wakati gani, kujuulikana khasa? Waambie: Ujuzi wa wakati wake uko kwa Mwenyewe Mola wangu Mlezi peke yake. Haujui wakati wake mtu yeyote isipo kuwa Yeye. Itapo tokea kitisho chake kitakuwa kikuu kwa walioko mbinguni na ardhini! Wao wanakuuliza suala hili kama kwamba wewe una pupa ya kuijua! Basi wakaririe jawabu, na uwambie kwa kutia mkazo: Hakika kuijua hiyo Saa kuko kwa Mwenyezi Mungu, lakini aghlabu ya watu hawatambui hakika ya wasiyo yaona au wanayo yaona!