Baada ya hao tulio kwisha wataja na tukawagawa sehemu mbili, walifuatia waovu wakairithi Taurati kutokana na walio watangulia. Lakini hao hawakufanya yalio amrishwa humo. Kwani wao walishika starehe ya dunia badala ya Neno la Haki. Wakijiambia nafsi zao: Mwenyezi Mungu atatusamehe kwa tunayo yatenda! Wakitaraji maghfira, na ilhali kuwa yakiwajia kama yale waliyo yashika watayashika vile vile. Basi wao wamekuwa wameshikilia kuendelea na madhambi pamoja na kutaka kwao msamaha. Tena basi Mwenyezi Mungu anawatahayarisha kwa vile kutaka maghfira na huku wanaendelea na yao, akasema: Sisi tulichukua kwao ahadi katika Taurati - nao wameyasoma yaliomo humo - kuwa waseme kweli; nao wakasema uwongo! Na hakika neema za nyumba ya Akhera za wanao jikinga na maasi ni bora kuliko starehe za duniani! Basi je, mtaendelea na uasi wenu, wala hayaingii akilini mwenu kuwa neema hizo ni bora kwenu? Na mnakhiari badala yake hizo starehe za dunia?