Mwenyezi Mungu kwa kuudhika naye kwa uasi wake alimwambia: Nini kilicho kuzuia usimtukuze Adam, na hali Mimi nimekuamrisha ufanye hivyo? Iblisi akajibu kwa inda na kiburi: Mimi bora kuliko Adam. Umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo. Na moto ni mtukufu zaidi kuliko udongo.
Mwenyezi Mungu alimlipa kwa inda yake na kiburi chake kwa kumfukuza katika makao ya utukufu wake, na akamwambia: Teremka kutoka hapo baada ya kuwa katika pahala pa juu. Haikufalii ukapandwa kichwa na ukaasi humo! Toka huko, nawe umehukumiwa hizaya na udhalili!
Kwa kumchukia Adam na kumhusudu alisema: Kwa sababu ya kunihukumia kupotoka na kupotea, nakuapia nitawapoteza wana wa Adam wasiifuate Njia yako Iliyo Nyooka, kwa kutumia kila hila zinazo mkinika.
Na ninaapa, nitawatokelea mbele yao, na nyuma yao, na kuliani kwao, na kushotoni kwao, na kila upande ninao weza, nikitafuta kila kipengee cha kughafilika kwao au udhaifu wao, nipate kuwapotosha, hata wasiwe wengi wao wanao kuamini Wewe, kwa kuto shukuru neema yako.
Mwenyezi Mungu akazidi kuudhika, akamwambia: Toka kwenye makao ya ukarimu wangu, wewe ulio hizika kwa kiburi chako na uasi wako, na khatima yako ni kuhiliki tu! Na ninaapa nitaijaza Jahannamu kwa wewe na hao wana wa Adam watao kufuata nyote pamoja!
Na ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika makao ya ukarimu wangu, nayo ndiyo hiyo Bustani, mneemeke humo, mkila kila chakula mpendacho, isipo kuwa mti huu. Msiukaribie! Msije mkawa wenye kujidhulumu nafsi zenu kwa adhabu itayo kupateni kwa kuvunja amri.
Shetani akawazaini waivunje amri ya Mwenyezi Mungu, ziwavuke nguo zilizo wasitiri zikashifike tupu zao. Akawaambia: Mola wenu Mlezi hakukukatazeni mti huu ila ni kwa kuwa hataki muwe Malaika, au msije mkawa mnaishi milele, na neema yenu haikatiki daima katika makao haya!
Basi akawachochea kwa udanganyifu mpaka wakenda kula ule mti. Walipo uonja tupu zao zikafichuka, wakaingia wanakusanya majani ya miti kujisitiri tupu zao. Mola wao Mlezi akawakaripia, na akawatanabahisha makosa yao kwa kuwambia: Mimi sikukukatazeni mti ule, na nikakwambieni kuwa Shetani ni adui yenu wa dhaahiri, hakutakieni kheri?