Na hakika kwa ajili ya kubainisha Haki tuliwapa Kitabu, na tukakipambanua. Kitabu hicho kimekusanya ilimu nyingi, na ndani yake zimo hoja za Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu, na Ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu; na pia zimo sharia zake, maelezo ya Njia Iliyo Nyooka, na uwongofu wa kuifikilia. Na pia yamo ndani ya Kitabu hichi mambo ambayo, lau watu wakiyafuata watapata rehema. Na wala hawanufaiki kwacho ila wale ambao ni shani yao kuinyenyekea Haki na kuiamini.
Hakika wao hawaiamini hii Qur'ani, na wala hawangojei ila matokeo ambayo Mwenyezi Mungu ameyabainisha kuwa yatawapata wanayo ikataa! Na Siku yatapofika hayo matokeo, nayo ni Siku ya Kiyama, walio ziacha amri zake na maelezo yake, na wakaghafilika kuwa ni waajibu kuiamini, na hali wakiungama madhambi yao, watasema: Hakika walikuja Mitume kutoka kwa Muumba wetu na Mlezi wetu, wakituitia Haki waliyo tumwa kuileta, nasi tukaikataa! Nao wataulizwa: Je, mnao waombezi wakakuombeeni? Nao hawatowapata! Au, je, watarudishwa tena duniani watende mema? Hawatajibiwa! Wamepoteza vitendo vyao kwa kukhadaika na dunia, na umewapotea ule uzushi wa uwongo wa kudai kuna mungu asiye kuwa Allah, Mwenyezi Mungu.
Hakika Mola Mlezi wenu ambaye Mitume wake wanakuiteni mwende kwenye Haki, na kuiamini Siku ya Mwisho na Malipo, ndiye Muumba ulimwengu, naye ndiye aliye uanza. Kaumba mbingu na ardhi kwa viwango sita, vinavyo shabihiana na siku sita, katika siku za dunia. Kisha akatawala juu ya Ufalme ulio kamilika. Naye ndiye anaye ufanya usiku uufunike mchana kwa kiza chake, na usiku unafuatia mchana kwa upesi na mpango na kufuatana kusikosita, kama anavyo taka Yeye. Naye Mwenyezi Mungu Subhana ameliumba jua, na mwezi, na nyota. Na vyote hivyo vinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu, vinakwenda kwa amri yake. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye kuumba na Mwenye amri ya kuitikiwa. Baraka za Mwenye kuanzisha ulimwengu na viliomo ndani yake zimetukuka. Aya hii tukufu imekusanya maana tatu: Ya kwanza ni kuwa mbingu na ardhi ameziumba Mwenyezi Mungu Mtukufu mnamo siku sita. Na hizi siku sio muradi wake hizi tuzionazo sasa, na tunazo zihisabu. Bali muradi wake ni kubadilika hali, baina ya giza totoro, na giza-giza la alfajiri, na mpambazuko wa asubuhi, na mchana, na adhuhuri, na jioni. Na haya yamekusanya hali sita zinazo badilika. Na giza-giza la magharibi linakitangulia kiza cha usiku. Na hizo hali sita au vipindi sita, ambavyo vimeitwa "siku" ndivyo wanavyo vitaja wanachuoni wa sayansi, navyo ni: Kipindi cha "Ether", kilicho elezwa katika Surat Ad-dukhan ya 44 ya kuwa ni moshi. Kisha kutokana na hiyo "Ether" yakatokea majua, ambayo moja lake ni hili jua letu. Kisha kutokana na jua zikawa sayari, na miongoni mwa sayari hizo ni hii dunia yetu. Tena katika ardhi zikawamo maadini mbali mbali. Tena ndio kikawa kipindi cha Ardhi, na baadae ukatokea uhai juu yake. Maana ya pili ya Aya hii ni kuwa kila kiliomo ulimwenguni kimo chini ya ufalme wa Mwenyezi Mungu peke yake, wala hapana ufalme usipo kuwa wake Yeye. Na nguvu zozote anazo pewa mtu hatoweza kuuendesha ulimwengu atakavyo. Ukomo wa uwezo wake ni kunufaika na vilivyo umbwa na akajua baadhi ya siri ziliomo ulimwenguni ambazo zilikuwa zimefichika. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu pekee ndiye aliye tuwa na kutawala juu ya A'rshi iliyo juu ya vyote vilivyo umbwa, na kwamba nyota na vitu vyote haviendi ila kwa amri yake peke yake. Maana ya tatu ni kuwa kupishana usiku na mchana kumetokea baada ya kwisha umbwa ardhi na mbingu. Basi hizo ni hali zenye kukhusika na asli ya uumbaji wa dunia, na makhusiano ya baina mbingu na ardhi na kuzunguka kwao na Mwenyewe Subhana Mwenye kuumiliki ufalme na utukufu na ukarimu.
Ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu, ndiye aliye umba kila kitu peke yake, basi muombeni Yeye tu kwa kumuabudu na kwa mengineyo, mkimtangazia hayo maombi, kwa udhalilifu na kunyenyekea, kwa dhaahiri au bila ya kudhihirisha. Wala msipite mipaka kwa kumshirikisha na wenginewe, au kwa kumdhulumu yeyote. Kwani hakika Mwenyezi Mungu, hawapendi wanao ruka mipaka, na wafanyao uadui.
Wala msifanye fisadi katika nchi njema kwa kueneza maasi na dhulma na uvamizi. Na muombeni Yeye Subhanahu, Aliye takasika, kwa kuiogopa adhabu yake, na kwa kutumai thawabu zake. Na hakika rehema yake ipo karibu kwa kila mwenye kufanya mema. Na hayo ni hakika.
Na Mwenyezi Mungu, Aliye takasika, Aliye tukuka, peke yake, ndiye anaye zipeleka pepo kubashiria rehema yake, kwa mvua ambazo kwa sababu yake ndio makulima humea, na konde humwagiwa maji. Hizo pepo hubeba mawingu ambayo nayo yamebeba maji. Tunayachunga mpaka yafike kwenye nchi isiyo kuwa na mimea, ambayo ni kama maiti asiye na uhai, yakamiminika maji, na tena Mwenyezi Mungu husabibisha kumea namna kwa namna ya mazao na matunda. Na mfano kama huu wa kuihuisha ardhi kwa mimea, ndivyo tunawafanya maiti wakawa wahai. Haya ni kwa ajili mpate kuikumbuka kudra ya Mwenyezi Mungu, na mpate kuamini kuwa kupo kufufuliwa.