Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu, nalo ni nguo hizi "maaddiy" za kuonekana, za kusitiri utupu, na nguo za "adabiy" zisizo onekana, bali ni za maana, nazo ni Taqwa, Uchamngu, katika kila pahala pa Swala, na kila wakati mnapo fanya ibada. Na jistarehesheni kwa kula na kunywa bila ya kufanya israfu au ubadhirifu, yaani kutumia kwa fujo, katika hayo. Basi msitumie vitu vilivyo harimishwa, wala msipite kiasi cha kiakili katika huko kujistarehesha. Hakika Mwenyezi Mungu hana radhi na wanao tumia kwa fujo.
Ewe Muhammad! Waambie kwa kuupinga ule uzushi wao kumzulia Mwenyezi Mungu juu ya kuhalalisha na kuharimisha: Nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo waumbia waja wake? Na nani aliye harimisha riziki iliyo halali na nzuri? Waambie: Hivi vitu vizuri ni neema inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Isingeli faa wastarehe navyo duniani ila wale walio amini, kwa sababu wao wanatimiza haki yao kwa shukrani na ut'iifu. Lakini rehema ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu, imewakusanya pia makafiri na wakhalifu katika dunia. Na Siku ya Kiama neema hizi zitakuwa za Waumini peke yao, wala hapana mwenginewe ataye shirikiana nao katika hayo. Na Sisi tunazieleza Aya, Ishara, zinazo onyesha hukumu kwa mpango huu ulio wazi kwa ajili ya watu wanao fahamu kwamba hakika Mwenyezi Mungu peke yake, Mwenye kumiliki kila kitu, ndiye Mwenye uwezo wa kuhalalisha na kuharimisha.
Ewe Muhammad! Sema: Hakika Mola wangu Mlezi ameharimisha mambo yaliyo zidi kwa ubaya, kama uzinzi; sawa sawa ukifanywa kwa siri au kwa dhaahiri. Pia ameharimisha kila maasi ya namna yoyote, na dhulma isiyo na njia ya haki. Na ameharimisha kumshirikisha na chochote kisicho kuwa na hoja madhubuti, au dalili ya kweli. Na pia kumzulia uwongo Subhanahu, Aliye takasika, katika kuhalalisha na kuharimisha, na mengineyo.
Na kila umma una ukomo wake maalumu. Na hapana uwezo wowote wa kuupeleka mbele mwisho huo au kuuakhirisha muda wake hata ukiwa mdogo vipi.
Enyi wanaadamu! Wakikujieni Mitume kutokana na hiyo jinsi yenu ya kibinaadamu kukufikishieni Ishara zangu zilizo funuliwa nyinyi mnakuwa makundi mawili. Kwa wale wenye kuamini na wakatenda mema kwa usafi wa niya, hapana khofu, wala wao hawatahuzunika katika dunia yao na Akhera yao.
Na wale wanao zikanusha hizo Ishara na wakapandwa na kiburi wasizifuate wala wasiongoke kwazo, basi hao ni watu wa Motoni. Humo wataadhibiwa daima milele katika adhabu.
Hapana wakubwa wa dhulma kuliko hao wanao mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa kumnasibisha na mshirika na mwana, na kuzua kuhalalisha na kuharimisha na mengineyo, pasina hoja. Au wanao kanusha Aya, Ishara, za Mwenyezi Mungu zilizo funuliwa katika Vitabu vyake na zinazo onekana katika ulimwengu wake. Hao wanapata hapa duniani sehemu ya aliyo waandikia Mwenyezi Mungu katika riziki, au uhai, au adhabu. Mpaka akiwajia Malaika wa Mauti kuzipokea roho zao, hapo huwaambia kwa kuwasuta: Iko wapi hiyo miungu yenu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu ije kukukingeni na mauti? Nao wajibu: Wametukataa, wametuacha na wametukimbia. Na wajishuhudie wenyewe wakikiri kuwa hakika walikuwa makafiri.