Adam na mkewe wakasema nao wamejuta wananyenyekea: Ewe Mola wetu Mlezi! Tumejidhulumu nafsi zetu kwa kuvunja amri yako, kuliko pelekea kuondoka kwa neema. Na ikiwa hutusamehe ukhalifu wetu, ukaturehemu kwa fadhila yako, hapana shaka tutakuwa katika wenye kukhasiri.
Mwenyezi Mungu akawaambia wao na pia na Shetani: Teremkeni nyote nyinyi, mtakuwa maadui nyinyi kwa nyinyi. Makao yenu na starehe yenu kwa muda mpaka ifike ajali yenu, yatakuwa katika ardhi.
Enyi Binaadamu! Sisi tumekuneemesheni. Tumekuumbieni nguo kusitiri tupu zenu, na vitu vya pambo. Lakini ut'iifu ndio nguo bora ya kukukingeni na adhabu. Neema hizo ni katika Ishara zenye kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu, na rehema yake, ili watu waukumbuke utukufu wake. Yeye tu ndiye anaye stahiki Ungu. Na kisa hichi ni katika nyendo za Mwenyezi Mungu za uumbaji wake, zinazo bainisha nini malipo ya kuvunja amri ya Mwenyezi Mungu, ili watu wakumbuke, na wafanye pupa kumt'ii Allah na kumshukuru.
Enyi wanaadamu! Msimuitikie Shetani na upotovu wake, mkatoka kwenye neema hizi, ambazo hazidumu ila kwa kushukuru na kut'ii, kama walivyo muitikia wazazi wenu, Adam na mkewe, akawatoa Shetani kwenye neema na ukarimu, na akawavua nguo zao zikaonekana tupu zao. Basi yeye Shetani na wasaidizi wake wanakujieni kwa namna msio watambua, wala hamuhisi mipango yao na vitimbi vyao! Lakini Shetani hana madaraka juu ya Waumini. Sisi tumemfanya yeye na wasaidizi wake kuwa ni marafiki wa wale wasio amini Imani ya kweli yenye kulazimikana na ut'iifu ulio timia.
Na wakanushao wakitenda jambo ovu la mwisho, kama shirki, na kut'ufu kwenye Al Ka'aba nao wako uchi, na mengineyo, basi wao hutoa udhuru kwa kusema: Sisi tumewakuta baba zetu wakenda mwendo huu huu, na sisi tunawafuata wao; na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hivi na ameturidhia kwa kuwa ametukiria! Waambie ewe Nabii kuwapinga kwa uzushi wao: Hakika Mwenyezi Mungu hakuamrisha mambo haya maovu! Je, mnamnasibishia Mwenyezi Mungu mambo msiyo kuwa nayo tegemeo lolote mnalo jua lina dalili ya ukweli wa kumnasibisha nalo Subhanahu?
Wabainishie aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, useme: Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu usio ingiliwa na uchafu. Na amekuamrisheni mumkhusishe Yeye tu kwa ibada kila wakati na kila pahala, na muwe wenye kumsafia niya katika hayo. Na nyote nyinyi baada ya kufa ni wenye kurejea kwake. Na kama alivyo anza kukuumbeni kwa wepesi, na mlikuwa hammiliki kitu chochote, basi kadhaalika mtarejea kwake kwa wepesi na hali mmeziacha nyuma ya migongo yenu neema zote mlizo nazo.
Siku ya Kiyama watu watakuwa makundi mawili:- Kundi moja lilio pata tawfiqi ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa lilichagua Njia ya Haki, likaamini na likatenda vitendo vyema. Na kundi jengine limehukumiwa upotovu, kwa sababu lilikhiari njia ya baat'ili, nayo ni ukafiri na uasi! Na hao walio potea waliwafanya mashetani ndio rafiki zao badala ya Mwenyezi Mungu, wakawafuata, nao wanadhani kuwa wao wamewafikiwa kwa kudanganyika kwao na khadaa za mashetani!