Na ardhi njema yenye rutba nzuri huzalisha mimea inayo kua kwa nguvu, kwa idhini ya Mola Mlezi. Na ardhi mbaya haitoi ila mimea michache, isiyo na faida, ambayo huwa ndio sababu ya dhiki ya huyo mkulima.
Washirikina wakafanya inda, na wakaikanusha Haki ilipo wajia kwa hoja za kukata zisio pingika. Lakini huo ndio mtindo wa makafiri kwa Manabii wao tangu zamani. Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake alio tokana nao. Naye akawakumbusha kuwa yeye ni mmoja wao: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake. Kwani nyinyi hamna Mungu asiye kuwa huyu. Na mjue kuwa kutakuwapo kufufuliwa na kuhisabiwa Siku ya Kiyama. Na hiyo ni Siku adhimu. Mimi nakukhofieni Siku hiyo msije mkapata adhabu kali kweli.
Wakasema wale wahishimiwa wao, watu wa mbele mbele na uwongozi katika wao, wakiujibu ule wito wake wa Tawhidi na Siku ya Akhera: Hakika sisi tunakuona wewe uko mbali kabisa na hiyo haki.
Nuhu akawaambia kukataa yale waliyo msingizia: Mimi sina upotofu kama mnavyo dai. Lakini mimi ni Mtume niliye toka kwa Muumba wa viumbe vyote, basi hayumkini awe mbali na haki.
Na mimi katika huu wito wa Haki mshike Tawhidi na kuamini Siku ya Mwisho, nafikisha Ujumbe aliyo nituma Mwenyezi Mungu, nao mfuate hukumu za Mwenyezi Mungu ambazo ndizo zinazo msilihi mwanaadamu. Na mimi nakupeni nasaha ya kweli itokayo kwenye moyo wangu ulio safi. Na Mwenyezi Mungu amenifunza mambo ambayo nyinyi hamyajui.
Mnanizulia kuwa nimepotea na kuwa nipo mbali na Haki? Na mnastaajabu kukujieni kumbusho kutokana na Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni kwa ulimi wa mtu aliye kuja kwenu kukuonyeni adhabu pindi mkikanusha, na akakuiteni mwende kuufuata uwongofu, na kutengeza nyoyo, na kujiepusha na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kutaraji muwe katika rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu duniani na Akhera? Haifai kuwa mnastaajabu na mnakanusha juu ya kuwepo hoja zenye kuthibitisha Utume huu.
Lakini wao juu ya hoja hizo zilizo wazi wengi wao hawakuamini, bali walimkanusha. Kwa hivyo tukawateremshia adhabu ya kuwazamisha katika maji, na tukawaokoa wale walio amini katika jahazi alilo liunda kwa kuongozwa nasi. Na wakazama wale walio kanusha juu ya kuwapo hoja zilizo wazi, nao wakafanya inda wakawa hawaioni Haki kwa kuwa walipofuka wasiione.
Kama tulivyo mtuma Nuhu kwa kaumu yake kuwalingania Tawhidi, kadhaalika tuliwatumia kina 'Aad Nabii Huud,naye ni mmoja wao, makhusiano yake nao ni kama ndugu kwa ndugu. Akawaambia: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake, nanyi hamna Mungu asiye kuwa Yeye. Na hii ndiyo njia ya kujikinga na shari na adhabu. Nayo ndiyo Njia Iliyo Nyooka. Basi je, mtaifuata njia mjikinge na shari na upotovu? 'Aad ni katika kabila yenye nguvu katika matumbo ya Taifa la Sam, na ni katika mat'abaka ya kwanza katika Waarabu wa jangwani. Ama makaazi yao yalikuwa katika Al-ah'qaaf iliyo tajwa katika Kitabu kitukufu katika Sura ya Al-ah'qaaf Aya 21. Wamewafikiana wanachuoni wa Kiislamu wa kutegemewa kuwa hiyo Ah'qaaf ipo katika nchi ya Yaman, ijapo kuwa wamekhitalifiana kidogo wapi khasa pahala penyewe. Kwa mujibu wa Yaaqut Al-h'amawy ni bonde baina ya Oman na nchi ya Mahara. Na kwa mujibu wa Is-haaq akimnukulu Ibn Abbas na Ibn Khaldun ni sehemu ya mchanga baina ya Oman na Hadhramaut. Kwa mujibu wa Qutaada ni sehemu ya mchanga karibu na bahari katika Shajar katika nchi ya Yaman. Na yafaa kutaja kuwa nchi ya 'Aad kwa mujibu wa baadhi ya Wamagharibi wa zamani ipo pande za juu za Hijaz katika jimbo la Husmaa, na karibu na makaazi ya Thamud. Vyo vyote ilivyo si mbali kuwa hao kaumu ya 'Aad walisafiri wakahamia jimbo hili wakati mmoja wapo.
Wakasema wenye uwongozi na umbele mbele katika kaumu yake: Sisi tunakuona umepungukiwa na akili, kwa kutuitia wito huu; na tunaitakidi kuwa wewe ni mwongo.
Akasema: Enyi watu wangu! Katika wito huu sina upungufu wa akili hata chembe, wala mimi si mwongo. Lakini mimi nimekuja na uwongofu, na mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, naye Yeye ndiye Mola Mlezi wa viumbe vyote.