Na mimi pupa yangu ni kumsemea kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na nimekujieni na Ishara yenye shani kubwa, yenye hoja iliyo dhaahiri katika kubainisha Haki niliyo kuja nayo. Basi waachilie waje nami Wana wa Israili, na uwatoe kwenye utumwa wa kahari yako, wende nami kwenye nchi nyengine isiyo kuwa yako, na huko wapate kumuabudu Mola Mlezi wao na wako.
Firauni akamwambia Musa: Ikiwa umekuja na Ishara (muujiza) kutokana na huyo aliye kutuma, basi nionyeshe kama wewe ni katika watu wakweli wanalo lishika neno la haki.
Kiasi ya Musa kuitupa fimbo aliyo kuwa nayo mkononi mwake wa kulia mbele ya Firauni, mara hiyo fimbo ikawa nyoka khasa dhaahiri, anakwenda mbio huku na huku, kwa nguvu zinazo onyesha kuwa ana uhai timamu.
Musa alipo ionyesha Ishara ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, zilitibuka roho za wapambe wa Firauni na waheshimiwa wa kaumu yake, wakasema katika kujipendekeza kwa Firauni na kumtetea: Hakika huyu ni bingwa katika ilimu ya uchawi, wala hii si Ishara itokayo kwa Mwenyezi Mungu!!
Na yeye ameelekeza lengo lake akupokonyeni ufalme wenu, na akutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake na yatayo tokea hapo kwa kuwavutia watu wamili na wamfuate. Basi tazameni, mnaamrisha njia gani ya kutokana naye huyu?
Wakasema: Akhirisha kukata shauri juu yake na nduguye huyu anaye msaidia katika wito wake, na watume watu katika askari wako wende katika miji ya ufalme wako wawakusanye walio mafundi katika ilimu ya uchawi.
Basi wakaja kwa Firauni wachawi walio kusanywa na askari wake. Nao wakasema: Hapana shaka nasi tutapata malipo makubwa yanayo lingana na hili linalo takikana kwetu, ikiwa sisi tutamshinda Musa.
Kisha wachawi wakamgeukia Musa, baada ya Firauni kuwaahidi alivyo waahidi, na wao wakaonyesha wana imani na nafsi zao na kujitayarisha kwao kwa uchawi wao katika uwanja wa mapambano. Wakamwabia: Ama utupe ulicho nacho kwanza, au sisi tuwe wenye kutupa tulicho nacho.
Musa akwajibu jawabu ya mwenye imani ya kushinda, akionyesha kutowabali: Tupeni nyinyi kwanza hicho mnacho tupa. Walipo tupa kila mmoja wao, navyo ni kamba na fimbo, macho ya watu yalizugwa, na ikawapitikia kuwa walicho kifanya kile ni hakika kweli. Na hali haikuwa ila ni kiini macho tu. Mambo yale yaliwatisha watu, na nyoyo zao zikaingia khofu na kitisho. Kwani wachawi wale waliwaletea watu uchawi unao onekana ni mkubwa, na athari yake katika macho yao ni kubwa!
Mwenyezi Mungu akaitoa amri yake kumpelekea Musa: Tupa fimbo yako. Sasa umekwisha fika wakati wake. Akaitupa kama alivyo amrishwa. Mara hiyo fimbo ikaingia kuvimeza vile vizushi vyao walivyo zua na kubuni!