Hao hakika wamejikubalia wenyewe wahisabike katika walio bakia nyuma, nao ni wanawake, na wasio jiweza, na watoto wadogo wasio viweza vita. Na Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao kwa khofu na unaafiki. Basi hao hawafahamu vilivyo uhakika wa Jihadi na kumfuata Mtume, nako ni kupata utukufu duniani na kupata radhi ya Mwenyezi Mungu katika Akhera.
Hiyo ndiyo hali ya wanaafiki. Lakini Mtume na wale walio sadiki pamoja naye, wametoa mali zao na roho zao ili kumridhi Mwenyezi Mungu, na kulinyanyua Neno lake. Hao tu peke yao ndio watakao pata kila kheri ya duniani, nayo ni utukufu na ushindi, na a'mali njema. Na wao peke yao ndio wenye kufuzu.
Na Mwenyezi Mungu amekwisha watengenezea katika Akhera neema za kudumu, katika Mabustani yanayo pitiwa na mito. Na huko ndiko kufuzu adhimu, na kufanikiwa kukubwa.
Na kama walivyo bakia nyuma baadhi ya wanaafiki katika Madina wasitoke kwenda pigana Jihadi, kadhaalika walikuja baadhi ya Mabedui, nao ni watu wa majangwani, wakijidai kutoa udhuru huu na huu ili waruhusiwe wabaki nyuma. Na kwa hivyo wakakaa nyuma wale walio mwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuonyesha Imani. Hawakuhudhuria, wala hawakumtaka udhuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ni dalili ya ukafiri wao. Adhabu ya kutia uchungu itawateremkia walio makafiri kati yao.
Hakika wanao kubaliwa udhuru wao kubaki nyuma ni wanyonge, na madhaifu wasio jiweza, na wagonjwa, na mafakiri wasio pata cha kutumia kujizatiti kwa vita. Na watu hawa wakiwa wao wana usafi wa niya kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika Dini yao, basi hao ni watu wema, wala hapana lawama juu ya watu wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Maghfira, na Mkunjufu wa Rehema.
Na kadhaalika hapana lawama juu ya Waumini wanao kujia uwapatie kipando cha kwendea Jihadi ukawaambia: Sina cha kukupandisheni. Wakenda zao na macho yao yanatiririka machozi kwa huzuni ya kukosa sharafu ya Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, kwa kukosa kwao masurufu ya kutoa.
Lawama na adhabu ni juu ya wale wanao kutaka ruhusa, ewe Mtume, wabakie nyuma wasende vitani, nao wanayo mali na zana, na wanaweza kutoka pamoja nawe. Kwani hao juu ya uwezo wao wamekhiari wabaki nyuma pamoja na wanawake wanyonge, na wazee wakongwe, na wagonjwa wasio jiweza; na nyoyo zao hao zimefungwa hazitambui Haki, na hawajui matokeo maovu kabisa yatakayotokea duniani na Akhera kwa kule kuacha kutoka kwao kwenda kwenye Jihadi.