Na pia Mwenyezi Mungu aliwafadhili wale wanaume watatu walio baki nyuma wasitoke kwenda kwenye Jihadi katika vita vya Tabuk. Hawa hawakubaki nyuma kwa unaafiki. Ilikuwa inatarajiwa Mwenyezi Mungu atoe bayana ya hukumu yao. Ilivyo kuwa toba yao ni ya kweli, na majuto yao makubwa hata wakaiona dunia nyembamba juu ya upana wake, na nafsi zao zikaingiwa na dhiki kwa hamu na huzuni, na wakajua kuwa hapana pa kuikimbia ghadhabu ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa kumwomba Yeye msamaha na kurejea kwake. Hapo basi Mwenyezi Mungu aliwaongoa watubu. Na Yeye akawasamehe, ili wapate kuendelea na hali ya toba. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba za wenye kutubu, ni Mwingi wa kuwarehemu waja wake.
Enyi mlio amini! Simameni imara baraabara juu ya uchamungu na Imani. Na kuweni pamoja na wale walio wakweli katika kauli yao na vitendo vyao.
Haikuwa ni halali kwa wakaazi wa Madina na majirani zao katika wakaazi wa majangwani kubaki nyuma wasitoke kwenda vitani pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. Wala kujifanyia uchoyo kwa ajili ya nafsi zao katika aliyo jitolea Mtume nafsi yake. (Mtume kajitolea roho na mali kwa kupigania Haki.) Kwani wao hakiwapati, katika Njia ya Mwenyezi Mungu, kiu, au machofu, au njaa, wala hawashuki pahala panapo watia ghadhabu makafiri, wala hakiwasibu kutokana na adui chochote kama kushindwa au kunyan'ganywa ngawira, ila huhisabiwa kwa hayo yote kuwa ni a'mali njema, ya kulipiwa bora ya malipo. Na Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wenye kufanya mema katika vitendo vyao.
Na kadhaalika Mujaahidina hawatoi mali wanayo toa, kingi na kidogo, wala hawasafiri safari yoyote, kwa Njia ya Mwenyezi Mungu ila huandikiwa katika madaftari ya vitendo vyao vyema, ili wapate malipo wanayo stahiki kuyapata hao watendao.
Haifai Waumini watoke wote kwenda kwa Mtume s.a.w. ila iwe dharura. Itakikanavyo ni kutoka kikundi kwenda kwa Mtume kwa ajili ya kusoma Dini, na wapate kuwaita watu wao kuwaonya na kuwabashiria, pale wanapo rejea. Haya ili wapate kuwa imara daima juu ya Haki, na watahadhari na upotovu na uharibifu.