Hakika hali yenu, enyi wanaafiki, ni kama hali ya wenzenu walio kutangulieni katika unaafiki na ukafiri. Kwa hakika wao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko nyinyi, na walikuwa na mali zaidi na watoto. Wakajistarehea kwa sehemu yao ya dunia walio jaaliwa, na wakapuuza kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kumcha Yeye. Na wakawakabili Manabii wao kwa kuwabeua na kuwakejeli. Na nyinyi mmejistarehea vile vile kwa mlivyo jaaliwa katika ladha za kidunia, kama walivyo jistarehea wao. Na nyinyi mkabobea katika mambo machafu na mapotovu kama walivyo bobea wao. Hakika hao vitendo vyao vimeharibika, basi havikuwafaa duniani wala Akhera, na wakawa wenye kukhasiri. Na nyinyi ni mfano wa hao katika hali na matokeo maovu.
Basi je, hawazingatii wanaafiki na makafiri hali ya walio watangulia katika kaumu ya Nuhu na A'ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Shuaib na kaumu Lut'? Mitume wa Mwenyezi Mungu waliwajia na hoja zilizo wazi wazi kutokana na Mwenyezi Mungu, na wakawakanusha na wakawakataa! Mwenyezi Mungu akawashika kila mmoja wao kwa dhambi zake, na akawateketeza wote! Wala Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini walizidhulumu wenyewe nafsi zao kwa ukafiri wao, na uasi wao kumuasi Mwenyezi Mungu, na wakastahiki peke yao kupata adhabu. Basi wao ndio wanao jidhulumu wenyewe.
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake, wao kwa wao ni wapenzi wa kupendana na kusaidiana, kwa mujibu wa Imani. Wanaamrisha yanayo amrishwa na Dini yao ya Haki, na wanakataza yanayo katazwa na Dini. Wanatimiza Swala kwa nyakati zake, wanatoa Zaka kuwapa wanao stahiki kwa wakati wake. Na wanat'ii anayo waamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wanayaepuka anayo yakataza Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hao ndio watakao kuwa chini ya Rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwalinda kwa Rehema, na Mwenye hikima katika upaji wake.
Mwenyezi Mungu amewaahidi hao Bustani (Pepo) watakao kaa daima katika neema zake, na makaazi ya kuziliwaza nafsi zao katika makao ya kudumu milele. Na pamoja na hayo watapata Radhi ya Mwenyezi Mungu kuwa radhi nao, nayo wataiona. Na hiyo ndiyo neema kubwa kabisa. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.