Sifa za wale walio uza nafsi zao kwa ajili ya Pepo ni kuwa wanakithirisha toba kwa Mwenyezi Mungu kwa kujikwaa kwao, na wanamhimidi katika kila hali, na wanakimbilia kwenda kujifanyia kheri nafsi zao na kuwafanyia wenginewe, na wanahifadhi Swala zao, na wanazitimiza kwa ukamilifu na unyenyekevu, na wanaamrisha kila kheri inayo wafikiana na Sharia ya Mwenyezi Mungu, na wanakataza kila uovu unao zuiliwa na Dini, na wanaishika Sharia ya Mwenyezi Mungu. Ewe Mtume! Wabashirie kheri Waumini!
Haimfalii Nabii na Waumini kuwatakia maghfira washirikina, hata ikiwa ni jamaa zao wa karibu kabisa, baada ya kwisha hao Waumini kuwajua kwamba hao washirikina wamekufa katika ukafiri. Kwani hao wamestahiki kukaa milele Motoni.
Haikuwa vile alivyo fanya Ibrahim a.s. kumtakia msamaha baba yake ila ni kutimiza ahadi aliyo ahidi Ibrahim kumuahidi baba yake, kwa kutaraji kuwa atakuja amini. Ilipo kwisha mbainikia Ibrahim kuwa huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu kwa kushikilia kwake ushirikina mpaka akafa na ukafiri, Ibrahim alijitenga naye, na akaacha kumwombea maghfira. Na Ibrahim alikuwa mwingi wa kuomba, na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, na mstahamilivu kwa maudhi.
Na si katika mwendo wa Mwenyezi Mungu na upole wake kwa waja wake kuwachukulia watu kuwa wamepotea, na awapitishie hukumu ya kuwatia khatiani na kuwapa adhabu, baada ya kwisha waongoza njia ya Uislamu, mpaka awabainishie kwa njia ya wahyi, ufunuo, kwa Mtume wake mambo ambayo inawapasa wajiepushe nayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema kila kitu.
Hakika ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mmiliki wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na Yeye ndiye Mwenye kuvisarifu viliomo humo kwa uhai na mauti. Na nyinyi hamna ila Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kutawala mambo yenu, wala hamna Msaidizi mwingine wa kukunusuruni na kukulindeni.
Mwenyezi Mungu Subhanahu amemfadhili Nabii wake na Masahaba wake wenye kuamini, walio wakweli, miongoni mwa Wahajiri na Ansari, walio toka pamoja naye kwenda pigana Jihadi wakati wa shida. (katika vita vya Tabuk) . Aliwaweka imara na akawalinda wasikhitalifiane, baada ya shida ya dhiki ya kuwafarikisha baina yao, hata zikakaribia nyoyo zao kuelekea kutaka kubaki nyuma wasitoke kwenda kwenye Jihadi. Tena Mwenyezi Mungu aliwasamehe kwa ile raghba yao iliyo wapitia ndani ya nafsi zao. Hakika Yeye Subhanahu ni Mwenye upole mwingi, na Mwenye rehema kubwa. Vita hivi vilikuwa mwezi wa Rajab mwaka wa 9 wa Hijra, baina ya Waislamu na Warumi. Na huitwa "Vita vya Dhiki", Ghazwatu U'sr, kwa sababu ya dhiki ya Waislamu waliyo kuwa nayo kwa ukosefu wa mali na zana. Katika vita hivi alijitolea Othman kulizatiti jeshi zima.