Katika haya ninayo kwambieni mimi nafikisha amri na makatazo ya Mola Mlezi wangu, na hayo ndio Ujumbe wake kwenu. Na mimi nakupeni nasaha ya dhati, kwa niya safi kabisa. Na mimi ni muaminifu katika ninayo kwambieni, wala mimi si miongoni ya watu waongo.
Tena Hud akawaambia: Hivyo mmestaajabu mno, na mkaona mageni kukujieni ukumbusho wa Haki kwa ulimi wa mtu aliye mmoja wenu, kukuonyeni? Mkiendelea na haya mliyo nayo matokeo yake yatakuwa ni mabaya mno. Na hakika jambo hilo si la kustaajabiwa. Kisha Huud akawatajia yaliyo wasibu walio kanusha katika watu walio watangulia, na akawakumbusha neema za Mwenyezi Mungu juu yao. Akasema: Kumbukeni Mwenyezi Mungu alivyo kufanyeni ndio warithi wa nchi baada ya kaumu ya Nuhu alio waangamiza kwa kumkadhibisha Nuhu, na Mwenyezi Mungu akakuzidishieni nyinyi nguvu za mwili na nguvu za utawala. Na neema hizo zinatakikana zilete Imani. Basi zikumbukeni neema zake ili mpate kufuzu.
Lakini wao juu ya wito mzuri huu walisema kwa kuona mageni: Hivyo wewe umetujia kututaka tumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja peke yake, na tuache masanamu waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Na hapana shaka sisi hatutofanya hayo, nawe tuletee hiyo adhabu unayo tutishia, kama wewe kweli ni katika wasema kweli!
Hakika kwa hii inadi yenu mmestahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu ikuteremkieni, na ghadhabu yake ikufikieni! Nyinyi mnabisha kwa ajili ya masanamu ambayo mliyo yaita kuwa ni miungu nyinyi na baba zenu, na wala si chochote ila ni majina tu walio pewa, na wala Mwenyezi Mungu hakuleta hoja ya kuonyesha ungu wao. Hayo hayana nguvu za muumbaji inayo kuruhusuni kuyaabudu! Na ikiwa mtashikilia ukaidi huu basi ingojeeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, nami pamoja nanyi, sote tungoje nini kitakushukieni.
Basi Sisi tukamwokoa A'ad na walio amini pamoja naye kwa rehema yetu, na tukawateremshia makafiri cha kuwateketeza, na hapana chao kilicho bakia wala hapana athari yao, na wala hawakuingia katika kundi la Waumini.
Na tuliwapelekea kina Thamud ndugu yao Swaleh, ambaye ni mwenzi wao kwa nasaba na uwananchi. Na wito wake ulikuwa kama wito wa Mitume walio kuwa kabla yake na baada yake. Akawaambia: Msafishieni ibada Mwenyezi Mungu peke yake, na wala hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Na hoja ya Utume wangu imekwisha kukujilieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Nayo ni huyo ngamia mwenye sifa za pekee. Katika huyo ngamia pana hoja. Yeye ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, muacheni ale atakapo katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru isije kukupateni adhabu chungu. Thamud ni kabila ya Kiarabu iliyo kuwa Al Hijr, baina ya Hijaz na Sham karibu na Wadi Alquraa.