Lakini tabia ya Firauni na wasaidizi wake ni kuto thibiti juu ya Haki. Wepesi kurejea kwenye khiana na uasi. Hao ni watu wa kigeugeu! Ikiwajia kutononoka na neema - na mara nyingi huwa hivyo - wao wakisema: Sisi tunastahiki haya tuliyo nayo kuwapita watu wengineo! Na likiwasibu la kuwaudhi, kama ukame, au tauni, au msiba wa miili au riziki, wakiona yamewapata hayo kwa ukorofi wa Musa na walio pamoja naye. Na wanaghafilika kuwa dhulma zao, na fisadi zao ndizo zilizo pelekea kuja hayo yanayo wapata! Basi na watanabahi, na wajue kuwa ujuzi wa ukorofi wao uko kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye anaye wapatiliza kwa sababu ya vitendo vyao viovu. Yeye ndiye anaye wapelekea hayo yanao waudhi, wala si Musa na alio nao. Lakini wengi wao hawaijui Hakika ambayo haina shaka.
Na kwa hii fikra mbovu waliyo nayo wakaendelea na upinzani. Walisema walipo ona miujiza ya Musa: Wewe hata ukituletea kila namna ya Ishara zinazo onyesha ukweli wa wito wako, ili kutuachisha dini yetu, na tusiwafanye watumwa watu wako, sisi hatukusadiki wala hatukufuati.
Basi Mwenyezi Mungu aliwateremshia masaibu na balaa zaidi, kama tufani lilio funika mwahala mwao, na nzige walio kula kila mmea na mti ulio bakia, na chawa, yaani vijidudu vinavyo haribu matunda na kuteketeza wanyama na mimea. na vyura vilivyo enea vikafanya maisha yao dhiki, na vikachafua kila pahala, na damu iliyo sabibisha maradhi mengi, kama kupasuka mishipa ya damu katika mwili, na damu inayo najisisha kila pahala ikasabibisha presha, au kupasuka ikaleta kiharusi na kupooza, na kutokwa na mkojo wa damu kwa sababu ya kichocho na mfano wake, au ikawa inachanganyika na maji yao wanayo hitajia kunywa au kupikia. Mwenyezi Mungu aliwapatiliza na Ishara hizi zote zilio wazi! Nao wasiathirike, nyoyo zao zikabaki kuwa ngumu, na wenye kutakabari hawataki Imani wala kurejea kwenye Haki. Walikuwa watu walio bobea kwenye madhambi na ukosefu, kama ilivyo ada yao.
Katika kuzidi kigeugeu chao kama zinavyo badilika sababu, walikuwa kila ikiwashukia namna yoyote ya adhabu wakisema kwa shida na machungu yanayo wapata: Ewe Musa! Tuombee kwa Mola Mlezi wako, kwa vile alivyo kuahidi kuwa ukimwomba atakupa miujiza na atakuitikia dua, atuondolee adhabu hii. Na sisi tunakuapia kuwa ukituondolea basi bila ya shaka tutakuitikia na tutawaachilia wende nawe Wana wa Israili kama ulivyo taka!
Tulipo waondolea adhabu kila mara kwa muda wao mpaka mwisho wake ukisha huivunja ahadi yao, na huenda kinyume na kiapo chao, na hurejea yale yale waliyo kuwa nayo. Kwao wao hayo majaribio ya kuwaachisha maovu hayakuleta faida!
Tuliwateremshia nakama yetu. Tukawazamisha baharini kwa sababu ya kushikilia kwao kukanusha Ishara zetu, na hadi ya kutoyabali mafunzo ya Imani na ut'iifu yaliyomo katika hizo Ishara.
Tukawapa watu ambao walikuwa wakidharauliwa katika Misri, nao ni Wana wa Israili, ardhi alio ipa baraka Mwenyezi Mungu kwa kuifanya ina rutba na kheri nyingi, tangu mashariki mpaka magharibi yake. Neno jema la Mwenyezi Mungu likatekelezwa kwa ukamilifu, na pia ahadi yake ya ushindi kwa Wana wa Israili, kwa sababu ya kuvumilia kwao dhiki. Na tukayateketeza majumba ya fakhari, na kila majenzi, na chanja za mimea ya kutambaa, na bustani, na pandio za mizabibu, waliyo kuwa wakisimamisha na kujenga akina Firauni na watu wake! Hiyo ndiyo shani ya Mwenyezi Mungu, na ametimiza kweli ahadi yake kwa Wana wa Israili.