Watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni kwa kuwaambia: Sisi tumekwisha ona thawabu alizo tuahidi Mola Mlezi wetu kuwa ni kweli. Je, nyinyi hiyo adhabu aliyo kuahidini Mola Mlezi wenu mmeiona kuwa ni kweli? Nao watajibu: Naam, Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia watu wa Peponi na watu wa Motoni: Laana, yaani kunyimwa na kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, ndio malipo ya wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na upotovu.
Hawa madhaalimu ndio wanao wazuia watu wasende kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu wa Haki, nayo ndiyo Imani na kutenda mema; na wanaweka vikwazo, na shakashaka, ili hiyo Njia yende upogo iwapoteze watu wasiweze kuifuata. Na hao wanaikanusha Akhera hawaiogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na baina ya watu wa Peponi na watu wa Motoni patakuwa na pazia kuzuia kufikia kwenye Mnyanyuko - na hapo ni pahala palipo nyanyuka palipo juu. Watu katika bora ya Waumini na watukufu wao, watakuwa wanawaangalia khalaiki wote hao, na wanawajua wema na waovu kwa alama zinazo onyesha ut'iifu wao na uasi wao. Wataitwa watu wema kabla ya kuingia Peponi, na hali wao wanataraji kuingia humo, watawabashiria kwa Imani na utulivu na kuingia Peponi.
Macho ya hao Waumini yakigeukia upande wa watu wa Motoni baada ya wito huo, watasema kwa kitisho watacho kioni cha Moto: Ewe Mola wetu Mlezi! Usitutie pamoja na hawa madhaalimu walio dhulumu nafsi zao, wakadhulumu Haki, na wakawadhulumu watu!
Na wale watu wa daraja za juu katika Pepo, nao ni Manabii, na Mas'iddiqina, watawaita walio kuwa wakiwajua kwa sifa zao katika watu wa Motoni, wakisema kwa kuwalaumu: Huko kujumuika kwenu kwa wingi, hakukufaini chochote, wala huko kupanda kiburi kuikataa Haki kwa kutegemea ujamaa wenu na utajiri wenu. Na hivi sasa mnawaona hawa, nini hali yao na nini hali yenu.
Hao wanyonge mlio kuwa mkiwadharau, na mkaapa kuwa hayumkini Mwenyezi Mungu awateremshie rehema, kama kwamba nyinyi ndio mnao ishika rehema yake, wao wamekwisha ingia Peponi! Na Mola wao Mlezi atawaambia: Ingieni humo kwa amani. Hapana khofu juu yenu kwa jambo lolote litalo kupateni, wala hamtahuzunika kwa jambo mlilo likosa.
Na watu wa Motoni watawanadia watu wa Peponi kwa kuwaambia: Hebu twachilieni maji kidogo yatumiminikie sisi, au tugaieni kitu katika vyakula na mavazi na starehe nyengine alizo kupeni Mwenyezi Mungu Mtukufu! Nao watu wa Peponi watawajibu: Sisi hatuwezi kufanya hayo, kwa sababu Mwenyezi Mungu amezuia vyote hivyo wasipate watu wapinzani, walio mkanusha Yeye na neema zake katika dunia.
Hawa makafiri ndio ambao hawakufanya juhudi kutafuta Dini ya Haki, lakini ikawa dini yao ni kufuata pumbao na matamanio, ndio pumbao la kujipumbazia na upuuzi wa kuchezea, na maisha ya dunia na anasa zake zikawakhadaa, wakadhania hayo tu ndiyo maisha, na wakasahau kukutana nasi! Basi Siku ya Kiyama Sisi tutawasahau. Na wao hawato istarehea Pepo, na watauonja Moto, kwa sababu ya sahau yao kuisahau Siku ya Kiyama, na kuzikanusha Ishara zenye kubainika wazi, zinazo thibitisha Haki.