Na tuliwapelekea kina Thamud ndugu yao Swaleh, ambaye ni mwenzi wao kwa nasaba na uwananchi. Na wito wake ulikuwa kama wito wa Mitume walio kuwa kabla yake na baada yake. Akawaambia: Msafishieni ibada Mwenyezi Mungu peke yake, na wala hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Na hoja ya Utume wangu imekwisha kukujilieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Nayo ni huyo ngamia mwenye sifa za pekee. Katika huyo ngamia pana hoja. Yeye ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, muacheni ale atakapo katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru isije kukupateni adhabu chungu. Thamud ni kabila ya Kiarabu iliyo kuwa Al Hijr, baina ya Hijaz na Sham karibu na Wadi Alquraa.