Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika mambo mlio amrishwa na mlio katazwa. Na wacheni kuzozana na kukhitalifiana. Hayo ndiyo yanayo pelekea kupoteza nguvu na kushindwa. Na vumilieni mkipata shida za vita. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanao vumilia wakasubiri kwa kuwapa msaada na kuwaunga mkono, na kuwalipa malipo mema.
Wala msiwe kama wale walio toka kwenye majumba yao, nao wana ghururi (udanganyifu) kwa nguvu na neema walizo nazo, wakijifakhari na kujionyesha mbele za watu, wakitaka wasifiwe kwa ushujaa na ushindi, na wao huku wanapinga watu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaupinga Uislamu. Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitendo vyao kwa ujuzi na uwezo. Na Yeye atakuja walipa duniani na Akhera.
Na kumbukeni, enyi Waislamu! Pale Shetani alipo kuja kuwazaini hawa washirikina kwa kuwaonyesha kuwa wayatendayo ni mazuri kwa uchochezi wake, akiwaambia: Hapana mtu ye yote anaye weza kuwashinda. Na akawahakikishia kuwa yeye atawalinda, na kuwanusuru! Yalipo kutana makundi mawili katika vita, vitimbi vyake na uchochezi wake ukavunjika. Akarejea nyuma, na akajitoa nao, akaogopa Mwenyezi Mungu asimuangamize. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Na kumbuka ewe Mtume! Walipo sema wanaafiki miongoni mwa makafiri na wale wenye Imani dhaifu walipo kuoneni mmesimama imara: Hawa Waislamu wameghurika kweli na dini yao! Na hakika mwenye kumwakilisha Mwenyezi Mungu jambo lake, na akamuamini Yeye, na akamtegemea Yeye, basi hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu atamkifia amwondolee hamu yake, na atamnusuru na maadui zake. Kwani hakika Mwenyezi Mungu madaraka yake yana nguvu, naye ni Mwenye hikima katika mipango yake.
Na lau kuwa unaona, ewe Mtume, kile kitisho kikubwa, kinacho wateremkia hawa makafiri, wakati ule Malaika wanapo wafisha na kuwang'oa roho zao, nao wakiwapiga mbele na nyuma, na wakiwaambia: Onjeni adhabu ya Moto kwa sababu ya vitendo vyenu viovu!!
Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja wake kwa kuwaadhibu kwa madhambi waliyo yatenda. Bali huo ni uadilifu, kwa sababu hawawi sawa muovu na mwema. Basi kuadhibiwa kwake ni kwa vitendo viovu alivyo vitenda mwenyewe.
Hakika ada ya hawa washirikina, na shani yao katika ukafiri, ni kama shani ya Mafirauni na majabari wote walio baki walio kuwa kabla yao. Walizipinga Ishara za Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa madhambi yao. Wala Yeye si mwenye kuwadhulumu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu katika kutekeleza hukumu yake, na Mkali wa kumlipa anaye stahiki adhabu.