Na enyi Waislamu! Jueni kuwa katika mali ya makafiri mliyo yateka, hukumu yake ni kugawiwa mafungu matano. Fungu moja ni la Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa zake Mtume, na mayatima, nao ni watoto wadogo wa Waislamu waliofiwa na baba zao nao ni mafakiri; na masikini, nao ni wale Waislamu wenye haja; na msafiri, naye ni mwenye kukatikiwa safari yake ya halali. Na yaliyo khusishwa katika hiyo sehemu moja katika tano kuwa ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume hukhusishwa kwa maslaha ya umma kama anavyo pasisha Mtume katika uhai wake, au, baada ya kufa kwake, Imam. Na yaliyo baki katika ile Khumsi watapewa walio kwisha tajwa. Ama sehemu nne nyengine katika ghanima (ngawira), na Aya ikanyamaza kimya juu yake, ni za wale walio pigana. Basi jueni hayo, na myajue ikiwa mmemuamini Mwenyezi Mungu kweli, na mmeziamini Ishara tulizo mteremshia mja wetu, Muhammad, za kumthibitisha na kumsaidia, siku ya Mpambanuo, tulipo pambanua baina ya ukafiri na Imani, nayo ndiyo siku lilipo kutana kundi lenu na kundi la makafiri katika Badri. Na Mwenyezi Mungu Mwenye kudra kubwa juu ya kila kitu aliwapa ushindi Waumini juu ya uchache wao, kuwashinda makafiri juu ya wingi wao.
Na kumbukeni mlipo kuwa bondeni ng'ambo hii ya karibu na Madina, na wao makafiri wako ng'ambo ile ya mbali, na msafara wenye bidhaa mlio kuwa mnautaka uko karibu zaidi nanyi upande wa baharini. Na lau kuwa mmepeana miadi ya kukutana kwa kupigana basi msinge wafikiana hivyo. Lakini Mwenyezi Mungu kapanga mkutane bila ya miadi, na bila ya kutaka wao, ili apate kutekeleza jambo ambalo katika ujuzi wake limekwisha thibiti litokee tu, wala hapana jenginelo. Jambo lenyewe ni kuwa vitokee vita vitavyo pelekea nyinyi mshinde na wao washindwe. Ipate kuondoka shaka - wateketee wa kuteketea kwa hoja wazi ya kuonekana, nako ni kushindwa makafiri juu ya wingi wao; na wahuike Waumini kwa hoja iliyo wazi, nako ni kushinda kulio toka kwa Mwenyezi Mungu kuwapa Waumini wachache. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na kujua. Haimfichikii kauli wala niya yoyote ya pande zote mbili.
Na kumbuka, ewe Mtume! Pale Mwenyezi Mungu alipo kufadhili kwa kukuonyesha usingizini ndoto ya kuwa hilo jeshi la maadui ni dogo, ili akutulizeni nyoyo muamini kuwa mtawashinda, kwa hivyo muwe imara kuwakaabili. Na lau angeli kuacheni muwaone wengi, bila ya kukuthibitisheni kwa ndoto hiyo, mngeli waogopa, na mkasita sita kupigana nao, na mngeli emewa, na mkazozana msonge mbele au mrudi. Lakini Mwenyezi Mungu amekuvueni na hayo, na akakuokoeni na matokeo yake, kwani hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo ndani ya vifua vya watu.
Na kumbuka, ewe Mtume! Alipo kuonyeshemi Mwenyezi Mungu kuwa maadui zenu mnapo kutatana nao ni wachache katika macho yenu, kama alivyo waonyesha wao kuwa nyinyi ni wachache, na kwa kuwa tangu hapo wao wana ghururi ndani ya nafsi zao kuwa ni wengi, ili kila mmoja wenu awanie kupigana na mwenzie, na kwa hivyo yatimie aliyo kwisha yaamrisha Mwenyezi Mungu. Na ilikuwa hapana budi hayo yatimie. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio hurejea mambo yote ya ulimwengu. Halitendeki jambo ila alilo kwisha lihukumia na kuzitengeneza sababu zake.
Enyi mlio amini! Mkikutana na kikosi cha wapiganaji katika adui zenu, basi kuweni imara, wala msiwakimbie. Na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa kufuata uwezo wake, na ahadi yake ya kuwasaidia Waumini, mkikithirisha kumkumbuka na kumtaja pamoja na kuwa imara na kusubiri. Mkifanya hivyo ndio matarajio yenu ya kupata mafanikio yatapo timia.